Shule hiyo ya msingi iliyoko katika mji wa Kwekwe, kiasi cha kilomita 200 kusini magharibi mwa mji mkuu wa Harare, shule iko jirani na migodi miwili ya dhahabu.
Katika siku zilizopita, uongozi wa shule ulilalamika kuhusu harakati za uchimbaji haramu wa madini unaofanywa chini ya viwanja vya shule.
"Msichana mmoja amejeruhiwa vibaya na mipango imefanywa kumkimbiza" hospitali, mbunge wa eneo hilo Judith Tobaiwa aliliambia shirika la habari la AFP.
Picha zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha shimo kwenye sakafu ya darasa, likiwa limemeza madawati, viti na mabegi ya shule.
Kwa jumla wanafunzi 17 wenye umri wa kati ya miaka 10 na 11 walijeruhiwa, mbunge Tobaiwa alisema.
"Bado wanaendelea na ulipuaji, majengo yote ya shule yanatikisika," aliongeza, wakati akizungumza kwa simu akiwa katika eneo la ajali.
Waziri wa maswala ya jimbo Larry Mavima alisema mamlaka iliamuru shule hiyo kufungwa na walikuwa wakijaribu kutafuta eneo jingine kwa ajili ya wanafunzi wake.
"Kama serikali tumeshtushwa sana na tukio hili na kusikitishwa kwamba wachimbaji madini hawakuchukua hatua stahiki kulinda eneo ili kuzuia ajali kama hiyo," alisema waziri huyo.
Zimbabwe ni nchi iliyoko kusini mwa Afrika isiyo na bandari inajivunia hifadhi kubwa ya dhahabu.
Ripoti ya 2020 ya Shirika la Kimataifa la Migogoro (ICG) ilikadiria kuwa watu milioni 1.5 wanajihusisha na uchimbaji mdogo mdogo wa madini kutokana na ukosefu mkubwa wa ajira, umaskini, na matatizo ya kiuchumi.
Chanzo cha habari hii ni shirika la habari la AFP.