Wafanyakazi wa uokoaji hawakupata manusura katika chumba cha uokoaji ndani zaidi ya mgodi wa zinki uliofurika nchini Burkina Faso, serikali na mmiliki wa mgodi walisema Jumanne, hakuna matumaini ya kwamba wachimba migodi wanane waliotoweka bado wanaweza kuwa hai baada ya mwezi mmoja.
Mgodi wa Perkoa, unaomilikiwa na kampuni ya Canada ya Trevali Mining Corp uliopo takriban kilomita 120 magharibi mwa mji mkuu Ouagadougou, ulididimia ghafla Aprili 16 baada ya mvua kubwa kunyesha bila kutarajiwa wakati wa msimu wa kiangazi nchini humo.
Kulikuwa na matumaini hafifu wakati wa operesheni ya mwezi mzima ya utafutaji na uokoaji kwamba watu waliopotea wanaweza kufika kwenye chumba cha uokoaji, ambacho kina chakula na maji na kilicho karibu mita 570 chini ya ardhi.
Vikosi vya uokoaji vimefungua chumba hicho cha hifadhi, kwa bahati mbaya ni kitupu, idara ya habari ya serikali ilisema katika taarifa iliyotumwa kwenye mitandao ya kijamii.