Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 16:23

"Wafanyakazi waliofukuzwa kudhoofisha sekta ya umma"


Rais John Magufuli
Rais John Magufuli

Uchambuzi wa orodha ya majina ya watumishi wa Umma wenye vyeti feki unaonyesha kuwa Halmashauri za Miji, Wilaya, Manispaa na Majiji zimeongoza kwa kuwa na dosari hiyo zikifuatiwa na taasisi za umma, hivyo huenda kufukuzwa kwao kutaacha pengo kubwa.

Baadhi ya wachambuzi wamesema kuwa kuondolewa kwa wafanyakazi hao serikalini kutaacha pengo kubwa hasa ukizingatia uzoefu na weledi walioupata kwa kutumikia serikalini kwa miaka mingi.

"Weledi hautokani tu na vyeti lakini pia uzoefu wa watendaji na uaminifu uliojengwa kwa muda mrefu katika taasisi hizi za umma," amesema mchambuzi wa masuala ya menejimenti ya umma akitaka jina lake lisitajwe.

Mchambuzi huyo amesema kuwa ingetafutwa busara na hekima ya namna ya kudhibiti kwa sasa mapungufu hayo badala ya kutumia njia za kisasi.

"Viongozi ni lazima wawe na huruma na wananchi wao na kuangalia chanzo na sababu zilizopelekea dosari zilizoko katika taasisi za umma katika kuchukua hatua," amesema.

Amesema hata ukileta nguvu kazi ya namna gani, bado unahitaji watu wenye uzoefu kuwaandaa hao vijana wanaotoka vyuoni, kinyume cha hivyo utazidi kutengeneza mapengo katika ufanisi wa shughuli za umma.

Kwa upande wake, wakili wa kujitegemea Mluge Karoli ameliambia gazeti la Habari Leo ingawa hatua hiyo itazalisha ajira lakini itatengeneza ukosefu wa ajira kwa upande mwengine.

"Unapowafukuza watu zaidi ya 9,000 unatengeneza watu ambao hawana ajira na wana wategemezi na wengine wanatarajia kustaafu karibuni.

"Ni jambo la kusikitisha kumfukuza mtu mwenye miaka 59 kazini bila haki zake wakati amefanya kazi vizuri."

Karoli aliongeza kusema kuwa ni vyema serikali ingeangalia namna nyingine kwa watu hao ila si kuwaondoa kwa kuwa waliondolewa wamefanya kazi kwa muda mrefu na wanaweza kufanya kazi vizuri kuliko wenye vyeti, hivyo njia nzuri ambayo ingepaswa kuchukuliwa ni kuangalia utendaji wao kuliko kujali zaidi vyeti vyao.

Ingetafutwa namna hasa ya kudhibiti kwa sasa kuliko kuwaondoa hao ambao wamefanya kazi kwa imani kubwa."

Vyombo vya habari kadhaa nchini Tanzania pia vimesema kuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHCR) Dkt Helen Kijo-Bisimba amesema: "Ni jambo zuri ambalo limefanyika lakini naona wasingewaondoa kazini badala yake wangeanzia hapa kwa kutengeneza mifumo ambayo itazuia kitu kama hicho kisitokee tena..."

Kwa upande wake Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Ally ameliambia gazeti la Habari Leo nchini Tanzania kuwa ili elimu iheshimike ifike mahali hatua hiyo iliyochukuliwa na Rais Magufuli iwaguse pia mawaziri, wabunge, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya.

Gazeti hilo pia limeripoti kuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu ambaye ni Mchumi Mtafiti, Profesa Haji Semboja alimwelezea rais Magufuli kuwa ni mtekelezaji na siye mtu wa maneno.

Profesa Semboja alisema mifumo ya zamani ilibidi itatue tatizo hilo katika ajira kwa kuwa haikuwa vizuri ndio maana hao watumishi wenye vyeti feki walifanikiwa kuingia. Alisema kila kiongozi anapokuja anakuwa na ajenda yake ya kimaendeleo, kwa Magufuli alikuja nah ii ya kuwa wenye vyeti stahili ndio wanaopaswa kukaa kwenye ajira.

“Wengi katika nafasi zao walikuwa hawakidhi vigezo hivyo walikuwa hawafanyi vizuri. Kwa sababu watanzania wengi hawana ajira sasa watapata na wale ambao hawana vyeti watakaa watafute utaratibu mwingine.

“Katika kosa hili wale watuhumiwa waliokamatwa ni moja ya matatizo ambayo yapo kwenye mfumo uliowaachia kufanya hivi,” alisema. Aliongeza kuwa kwa karne ya sasa kuna haja ya kuangalia katiba na sheria kuwa hao viongozi ambao hawajaguswa ni watumishi wa serikali hivyo wanapaswa kuwa na vyeti vya uhakika.

Naye Mtaalamu wa masuala ya sayansi ya siasa, Profesa Mwesiga Baregu alisema kitendo cha kuwa na watumishi wenye vyeti feki zaidi ya 9000 ni uzembe uliokithiri uliotokana na mfumo uliokuwepo.

Pia gazeti hilo limeandika alihoji kwa nini wengine wachukuliwe hatua hiyo na viongozi wengine waachwe, kwani jambo kama hilo linahitaji kufanywa kwa utaratibu. Maoni ya wanasiasa Kiongozi wa Chama cha ACT -Wazalendo na Mbunge wa Kigoma Mjini Kabwe Zitto (ACT – Wazalendo) alisema uhakiki wa vyeti ni hatua muhimu kusafisha utumishi wa umma kama utafanyika kwa usawa.

“Hata hivyo ni vizuri uhakiki huu kutobagua, hata wanasiasa na nafasi za kuteuliwa nao wafanyiwe uhakiki,” alisema Zitto. Zitto alisema isipofanyika hivyo wananchi wataona kuna ubaguzi na hivyo kujenga chuki dhidi ya wanasiasa na wateuzi ambao hawakuguswa na zoezi hilo.

Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi Taifa na Mbunge wa Jimbo la Vunjo, James Mbatia ameliambia gazeti la habari leo ana wasiwasi katika vigezo vilivyotumika kuwaondoa watumishi hao. “Sijui walipewa haki ya kusikilizwa maana hii ni haki ya msingi kwa binadamu, hata hivyo ujumbe wangu ni kwamba usianze jambo kabla hujajua athari yake,” alisema Mbatia.

Alisema mfumo wa elimu unaotumika hapa nchini unaweza kuwa sababu kubwa ya kuwepo kwa watu hao baada ya serikali kuruhusu mfumo huria wa elimu katika sekta binafsi ambapo mwaka 2013 alizungumzia udhaifu wa elimu inayotolewa hapa nchini.

Mbatia alisema kuna watoto ambao waliingia shule za binafsi na kurushwa madarasa baada ya uwezo wao kuonekana mzuri hivyo wapo ambao hawakufanya mtihani wa darasa la saba na pia wapo ambao hawakufanya mtihani wa kidato cha nne.

Aidha Mbatia alisema hata hivyo serikali kama imeamua kuwaondoa watu hao kazini ni vema ingewasafisha na viongozi wao ambao kwenye taarifa hiyo hawakuguswa ikiwa ni pamoja na wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya.

“Tutende haki basi, vinginevyo hii ni fujo na tutatengeneza chuki kwa watu kama na wao walidanganya kwanini na wao wasichukuliwe hatua, atawezaje kusimamia wengine kama na yeye siyo msafi?” alisema Mbatia.

Orodha iliotolewa na serikali imezitaja taasisi za umma zenye wafanyakazi wenye vyeti bandia ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambapo imeonyesha kuwa wafanyakazi wanane wanahusika.

Aidha mfuko wa Pensheni wa PPF wafanyakazi 16, Shirika la Ndege (ATCL) wafanyakazi 7, Shirika la Reli (TRL) wafanyakazi 24, Mamlaka ya Reli wafanyakazi 39 na Mamlaka ya Anga wafanyakazi 22.

Rais John Magufuli juzi alipokea repoti yenye orodha ya watumishi wa umma ambao kati yao wanadaiwa kuwa na vyeti pungufu au vyeti tata au vyeti vya kughushi.

Repoti hiyo ilitayarishwa na ofisi ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, chini ya usimamizi wa Angella Kairuki.

Hatua ya kufanyika kwa uhakiki huo ambayo ilitokana na agizo la Rais Magufuli inafanya sasa kuwepo kwa nafasi wazi za ajira 12,000.

Idadi hiyo inatokana pia na kubainika kuwepo kwa vyeti tata 3,076. Kwa mujibu wa orodha hiyo iliyotolewa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Dk Laurean Ndumbaro, halmashauri zina idadi ya wafanyakazi 8,716, huku taasisi za umma zikiwa na jumla ya wafanyakazi 1,216.

Wakati halmashauri za Mikoa ya Dar es Salaam na Tanga zinaonekana kuwa na idadi kubwa zaidi ya wafanyakazi wenye vyeti vya kughushi, mikoa ya Simiyu, Mbeya, Songwe, Shinyanga, Ruvuma, Tabora na Singida imekuwa na idadi ndogo zaidi ya wafanyakazi hao.

Kwa mujibu wa repoti hiyo vyuo vya elimu ya juu ambavyo ndio tegemeo katika kuzalisha wataalamu, baadhi vimebainika kuwa na idadi kubwa ya watumishi wenye vyeti bandia huku Chuo Kikuu cha Sokoine kikiongoza katika kundi hilo kikiwa na wafanyakazi 33.

Aidha kwa upande wa kundi hilo, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimekutikana na mfanyakazi mmoja tu aliyebainika kuwa na cheti bandia.

Pia vyeti feki vimekutikana katika Chuo cha Utumishi wa Umma ambapo imebainika kuwa na wafanyakazi 10, Chuo Kikuu cha Dodoma wafanyakazi watano, Chuo Kikuu cha Tiba na Afya Muhimbili wafanyakazi watano, huku Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam watumishi sita.

XS
SM
MD
LG