Klaus Mueller, mkuu wa wadhibiti wa nishati wa Ujerumani, alituma ujumbe wa Twitter, akieleza kwamba mtiririko wa gesi umefikia 40%, kiwango sawa na kile kilichokuwepo kabla ya ukarabati huo kuanza.
Kampuni ya Gazprom inayomilikiwa na serikali ya Russia inadai kwamba kiwango cha gesi kimepungua kwa sasabu mtambo uliokuwa ukifanyiwa ukarabati nchini Canada, haujarejeshwa.
Rais wa Russia Vladimir Putin amesisitiza kwamba Gazprom itatimiza majukumu yake, huku akionya kwamba kazi ya kukarabati mtambo huo mwingine, baadaye mwezi huu inaweza kusababisha kupungua kwa kasi ya usafirishaji wa bidhaa hiyo.
Viongozi wa Umoja wa Ulaya wametahadharisha juu ya uwezekano wa Russia kukatiza usafirishaji wa bidhaa hiyo, kwa ajili ya kukabiliana na shinikizo la nchi za Magharibi kwa Russia kwa sababu ya uvamizi wake nchini Ukraine.
EU imezitaka nchi wanachama kupunguza kwa hiari matumizi yao ya gesi, kutafuta njia mbadala na kuokoa gesi iliyopo kwa sasa, ili kutumika wakti wa msimu wa baridi.