Jammeh alitawala taifa hilo dogo la Afrika Magharibi kwa miaka 22, akiongoza serikali iliyotuhumiwa kutekeleza mateso, kutumia magenge yanayoua watu na kufanya dhulma nyingine nyingi.
Jammeh amekua akiishi uhamishoni nchini Equatorial Guinea tangu mwaka 2017 aliposhindwa katika uchaguzi na rais wa sasa Adama Barrow, lakini bado ana wafuasi wengi nchini mwake na ameonyesha mara nyingi nia ya kurejea kwenye siasa.
“Leo, nimeamua kuchukua chama changu mwenyewe na sitakikabidhi kwa mtu yeyote,” Jammeh alisema katika ujumbe wa sauti uliotumwa kwa wafuasi wake kutoka chama cha Alliance for Patriotic Reorientation and Construction (APRC) siku ya Jumatano.
“Kama kuna mtu yeyote anapenda au asipende, kwa neema ya Mwenyezi Mungu, nitarudi.”
Jammeh ametoa tangazo hilo mwezi mmoja baada ya Jumuia ya nchi za Afrika Magharibi ECOWAS kuiunga mkono mahakama maalum ya mseto kutoa hukumu kwa uhalifu uliotendwa wakati wa utawala wake.
Mwaka 2022 serikali ya Gambia iliidhinisha mapendekezo ya tume iliyochunguza ukatili uliofanywa chini ya Jammeh, huku maafisa wakikubali kuwashtaki watu 70 akiwemo rais huyo wa zamani, aliyeingia madarakani kufuatia mapinduzi ya mwaka 1994.
“Wacha wanaotishia kuniweka jela wasubiri nifike. Siku ya uwajibikaji imefika na itakuwa siku ya adhabu,” alisema dikteta huyo wa zamani.
Forum