Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Januari 22, 2025 Local time: 15:47

Rais Ruto avunja baraza la mawaziri


Rais wa Kenya William Ruto.
Rais wa Kenya William Ruto.

Rais wa Kenya William Ruto Alhamisi alilivunja baraza lake la mawaziri na kusema kwamba ataendelea kufanya mashauriano na wadau mbalimbali kuhusu masuala kadhaa yaliyoibua utata nchini humo katika siku za karibuni. 

Akilihutubia taifa kutoka ikulu mjini Nairobi, Ruto alisema ofisi ya makamu wake na ile ya mkuu wa mawaziri hazitaathiriwa na hatua hiyo ya hivi punde.

“Mimi kwa mujibu wa mamlaka niliyopewa na Ibara ya 152(1) na 152(5)(b) ya Katiba na kifungu cha 12 cha Sheria ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, nimeamua kufuta mara moja mawaziri na Mwanasheria Mkuu kutoka Baraza la Mawaziri la Jamhuri ya Kenya isipokuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Mawaziri na Waziri wa Masuala ya Kigeni na Diaspora," Ruto alisema.

Ruto alitangaza hayo wakati ambapo utawala wake umekuwa chini ya shinikizo kumtaka kujiuzulu kufuatia maandamano yaliyojumuisha vijana wa kizazi kipya maarufu kama Gen Z.

"Shughuli za serikali zitaendelea kama kawaida chini ya uangalizi wa makatibu wakuu wa wizara," alisema Rais Ruto.

Aliahidi kuunda timu mpya ambayo itamsaidia katika "kuharakisha utekelezaji wa lazima na wa haraka wa mipango ya kushughulikia mzigo wa madeni, kuongeza rasilimali za ndani, kupanua nafasi za kazi, na kukabiliana na jinamizi la ufisadi."

Forum

XS
SM
MD
LG