Haya yalijiri siku ambayo kundi hilo la nchi zilizositisha uhusiano na Qatar, zilipotoa taarifa ya pamoja na kuelezea kutoridhika kwao na majibu yaliyotolewa na Qatar dhidi ya shinikizo kwa taifa hilo.
Waziri Sheikh Mohamed bin Abdulrahman al-Thani aliwaambia waliohudhuria kikao mjini London kwamba Qatar inaamini kuwa msukumo wote huo unaongozwa na Saudi Arabia na Umoja wa falme za Kiarabu, na kwamba kuna haja ya kujua sababu halisi za kameni hiyo.
Matamshi hayo yamejiri mwezi mmoja baada ya nchi nne kusitisha uhusiano wa kidiplomasia na Qatar, kwa tuhuma kwamba nchi hiyo ya ghuba, ambayo ina utajiri mkubwa wa mafuta, inadhamini ugaidi. Qatar hata hivyo, imekanusha madai hayo.
Wakati Saudi Arabia na washirika wake wakiendelea kuwa katika mgogoro wa kidiplomasia na Qatar, walisema mapema Jumatatu iliopita kwamba wataongeza muda wa saa 48 ili Qatar iweze kutekeleza masharti yao.
Kuwait, ambayo imekuwa inajaribu kutafuta suluhu kwa njia ya amani ilikusaidia kushawishi mataifa ya ghuba ya uajemi kuondoa vikwazo dhidi ya Qatar, iliomba kuongezwa muda kuendelea kutafuta suluhu hadi Jumapili.
Kuwait iliomba muda zaidi, muda mfupi baada ya masharti yaliotolewa na muungano wa Saudi Arabia, ukiitaka Qatar iwe imewasilisha majibu, kukaribia kufikia kikomo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa wiki iliopita na mashirika ya habari ya Kuwait na Saudi Arabia, imethibitisha kwamba muda uliongezwa mpaka mwisho wa Jumatatu iliyopita.
Saudi Arabia, falme za kiarabu, Bahrain, na Misri zimetishia kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na kibiashara na Qatar toka Juni 5, zikishutumu serikali ya Doha kufadhili ugaidi na ushirika wake na Iran.