Trump aliukosoa vikali mswaada huo mapema wiki hii na kueleza Jumamosi kuendelea kwake kukataa kuusaini.
Trump aliandika katika Twitter Jumamosi, “Si jingine nataka watu wetu wapate dola za Marekani 2,000, na siyo kiwango kidogo cha dola 600 ambazo ziko katika mswaada. Pia, acheni ufujaji wa matumizi ya bilioni za dola.”
Malipo makubwa yanaonekana kuwa hayaendani na matakwa ya wanachama wa chama chake cha Republikan, ambao walizuia juhudi za Wademokrat kujadili kiwango kikubwa cha malipo.
Wamarekani milioni 14 watapoteza posho ya kutokuwa na ajira, kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Kazi.
Rais mteule Joe Biden alimtaka Trump kusaini mswaada huo.
“Huku kutokuwajibika kuna matokeo mabaya. … Mswaada huu ni muhimu. Unahitaji kusainiwa kuwa sheria hivi sasa,” Biden, ambaye anatumia muda wa mapumziko nyumbani kwake katika jimbo la nyumbani Delaware, amesema katika tamko lake.
Rais Donald Trump yuko katika mapumziko kwenye nyumba yake ya kifahari huko Florida wakati Wademokrat na Warepublikan wakingojea kuona iwapo atasaini sheria ya matumizi ya dola trilioni 2.3, inayojumuisha dola bilioni 892 za msaada wa janga la virusi vya corona. Mswaada huo ulipelekwa kutoka Washington hadi katika klabu yake ya Mar-a-Lago utakaotumika iwapo ataamua kusaini kuwa sheria.
Trump hakuonyesha wazi kutishia kuzuia muswada huo, lakini aliwashangaza wabunge katika vyama vyote viwili kwa kuuita ni “fedheha” baada ya kupitishwa katika Baraza la Wawakilishi na Baraza la Seneti, uliokuwa kwa miezi kadhaa ukijadiliwa.
Baadhi ya idara za Serikali kuu zitaanza kufungwa mapema Jumanne iwapo Trump hatasaini mswaada huo. Bunge lina mpango wa kurejea kufanya kazi Jumatatu, na kusitisha mapumziko ya sikukuu ya Krismas, na kuchukua hatua ya kujaza pengo kwa kupitisha fedha za kutumika siku chache au wiki kadhaa wakati ufumbuzi unatafutwa juu ya mswaada huo uliokwama.
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamepangiwa kupiga kura Jumatatu kubatilisha kizuizi alichoweka Trump juu ya muswada wa dola bilioni 740 unaoidhinisha programu za ulinzi wa Marekani. Iwapo kura za Baraza la Wawakilishi zitapita, Baraza la Seneti linaweza kupiga kura juu ya hatua hiyo mapema Jumanne. Unahitaji theluthi mbili ya kura katika mabaraza yote mawili kuweza kubatilisha kizuizi alichoweka rais.