Vurugu hizo nchini Afrika Kusini zilionekana kupungua Alhamisi, wakati polisi wa kulinda doria walikuwa wamepelekwa kufanya ulinzi mkali katika miji hiyo.
Wakati huohuo, baadhi ya wahamiaji walieleza wasiwasi wao juu ya kuendelea kuishi nchini humo.
Ofisi za ubalozi wa Afrika Kusini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zimekumbwa na vurugu, na huko Nigeria, vyombo vya usalama vinalinda doria katika eneo la ubalozi wa Afrika Kusini na biashara zinazomilikiwa na wananchi wa Afrika Kusini kufuatia maandamano na vitendo vya ulipizaji kisasi dhidi ya mashambulizi ya wananchi wa kigeni Afrika Kusini.
Katika hotuba yake Alhamisi, Rais Cyril Ramaphosa alilaani mashambulizi hayo yaliyoanza Jumapili, yaliohamasishwa na madereva wa magari makubwa na wengine ambao wanashikilia kuwa wahamiaji wamechukua fursa za kazi katika nchi yao.
“Hakuna kiwango cha hasira na manunguniko yanaweza kuhalalisha vitendo vya uharibu wa makusudi na uhalifu. Hakuna namna yoyote ya kuhalalisha mashambulizi haya katika makazi na biashara za raia hawa wa kigeni, kama ilivyokuwa hakuna udhuru wa namna yoyote unaokubalika kwa chuki dhidi ya wahamiaji au aina yoyoe ya kukosekana kuvumiliana,” amesema Rais.
Ramaphosa amesema kuwa zaidi ya watu 400 walikamatwa upande wa kaskazini mashariki ya jimbo la Gauteng, ambako jiji la Johannesburg na mji mkuu, Pretoria ndiko ilipo.