Polisi wa Misri na waandamanaji wamepambana katika miji iwili ya mashariki katika siku ya tatu ya maandamano ya kupinga serikali kote nchini humo.
Polisi walirusha mabomu ya machozi na risasi za mpira kwa waandamanaji hao huko Suez Alhamisi. Waandamanaji katika mji huo walichoma kituo cha Polisi na jengo la serikali jumatano usiku.
Waandamanaji wengine walijaribu kulipua makao makuu ya chama tawala cha National Democratic Party kabla ya Polisi kuwarudisha nyuma kwa mabomu ya machozi. Watu wapatao 55 walijeruhiwa kwenye ghasia hizo.
Wakati huo huo mamia ya waandamanaji walipambana na Polisi katika mji wa Ismailia.
Shirika la Associated Press lilimkariri mwanachama wa chama tawala Safwat El -Sherrif akisema kuwa serikali iko tayari kwa mazungumzo ya umma juu ya chuki ya Misri. Lakini mshirika wa karibu wa Rais Hosni Mubarak pia amesema kwa maneno yake kuwa “watu wachache wa nchini humo hawawezi kulazimisha matakwa yao kwa walio wengi.”