Pia wamesema wameimarisha zaidi ulinzi wa doria katika maeneo yalikotokea mauaji hayo na maandamano.
Serikali imewalaumu wanasiasa wanaohamasisha vitendo vya uvunjifu wa amani wakiwataka kuhubiri amani kinyume cha hivyo watakamatwa.
Wakazi wa eneo hilo la Riverside, lililoko Nairobi walichoma magari matatu ya umma na kuzuia barabara hiyo katika tukio hilo mapema Jumapili.
Wakati huohuo polisi nchini Kenya wamethibitisha kuwa watu watano waliuawa na kumi wengine kujeruhiwa na mali za raia kuharibiwa wakati wa vurugu zilizotokea Nairobi Jumamosi
Viongozi wa Muungano wa Upinzani, Nasa, wanaripotiwa na Mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili VOA kutembelea eneo hilo la Mathare ambapo mapambano yamekuwa yakiendelea kati ya polisi na waandamanaji baada ya mauaji ya watu watano.
Pia imeripotiwa kuwa Kiongozi wa Nasa Raila Odinga na timu yake wamemtembelea Mbunge wa Mathare Kaskazini Anthony Aluoch aliyejeruhiwa katika fujo hizo.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari watu kadhaa waliopata majeraha ya risasi tayari wamefikishwa hospitali na huenda idadi ya vifo ikaongezeka.
Kwa upande wake Rais Uhuru Kenyatta amesema kuwa :“Tunayo Katiba na tunaongozwa na tunaongozwa kama taifa na utawala wa sheria. Ni lazima tufuate hilo. Na kuwataka watu wafuate sheria siyo kwamba tunavuka mipaka.”
Rais amesema kuwa yeye hayuko juu ya sheria, akisema hivi karibuni alifanya uamuzi wa kuheshimu sheria alipotakwa na Mahakama ya Juu kurudia uchaguzi baada ya kubatilishwa matokeo ya Agosti 8 ambapo alitangazwa kuwa mshindi.
Amesisitiza Wakenya waendelee na utulivu kwani serikali yake haitakubali kuwepo machafuko na uvunjifu wa amani nchini.
Naye Makamu wa Rais William Ruto amewatuhumu Nasa kwa kutumia vitisho na vurugu kutaka kupata madaraka.
“Wao wanafikiri wanaweza kutumia vitisho na vurugu kupeleka mbele ajenda yao ya kisiasa na kuwa hawatofanikiwa. Hatuwezi kujisalimisha kwa watu wanaotumia vitisho na rushwa,” amesema.