Hisia mseto zimeendelea kutolewa kufuatia uamuzi wa jopo la mahakama moja ya jimbo la Florida kupendekeza kwamba Nikolas Kruz, mtu aliyekiri kuua watu 17 kwa bunduki katika shule moja kwenye jimbo hilo hatapata hukumu ya kifo.
Vyombo mbalimbali vya habari vya Marekani vimeripoti kwamba wanafamilia wengi wa wale waliopoteza maisha yao katika shambulizi hilo, hawakuridhia uamuzi huo wa Alhamisi.
Jopo hilo lilipendekeza Kruz ahukumiwe kifungo cha maisha gerezani bila nafasi ya kupewa msamaha, kwa mauaji ya 2018 ya wanafunzi 14 na wafanyakazi 3 katika Shule ya Upili ya Parkland, ya Marjory Stoneman Douglas.
Jaji wa mahakama hiyo, aliyesoma mapendekezo ya jopo hilo, alisema kwamba halikuweza kukubaliana kwa kauli moja kwamba anapaswa kunyongwa.
Pendekezo hilo lilikuja baada ya mashauriano ya saa saba, kwa muda wa siku mbili, na kumaliza kesi ya miezi mitatu iliyojumuisha video za picha, ushuhuda kuhusu mauaji hayo na matokeo yake, ikiwa ni pamoja na ushuhuda wa kuumiza moyo kutoka kwa wanafamilia wa waathiriwa.
Chini ya sheria ya Florida, hukumu ya kifo inahitaji kura ya pamoja kwa angalau hoja moja. Jaji wa Elizabeth Scherer atatoa hukumu hiyo baadaye.
Cruz, nywele zake zikiwa hazijachanwa, kwa kiasi kikubwa aliketi chini na kutazama meza wakati mapendekezo ya jopo la mahakama yakisomwa.
Wengi waliokuwa mahakamani, baadhi wakiwa ni jamaa za waathiriwa, walitikisa vichwa vyao, wakionekana kuwa na hasira au wakifunika nyuo zao, kuonyesha kutoridhika kwao na pendekezo hilo la kifungo cha maisha.