Rais Barack Obama wa Marekani amesema Jumapili Kenya na mataifa mengine ya Afrika ni lazima yazingatie nguzo za maendeleo ili kupata maendeleo ya kudumu barani humo.
Akihutubia maelfu ya wananchi wa Kenya katika uwanja wa Kasarani mjini Nairobi Rais Obama aliorodhesha mambo kadha ikiwa ni pamoja na kuzingatia misingi ya demokrasia, kujengea fursa vijana, kupambana na rushwa, kuhakikisha wanawake na wasichana wanapata fursa za kuchangia katika maendeleo ya taifa, na kuimarisha amani na usalama kama misingi ambayo italeta na kulinda maendeleo yanayopatikana.
Uwanja wa ndani wa Kasarani ulijaa maelfu ya Wakenya waliokuja kwa mwaliko kumsikilizi Rais Obama akitoa hutuba yake - tukio lake la mwisho nchini Kenya kabla ya kuondoka kuelekea Ethiopia baadaye Jumapili.
Ilikuwa kilele cha ziara yake ya siku tatu nchini humu na alitumia hotuba hiyo kuelezea hisia zake binafsi kwa nchi ya Kenya, akielezea historia ya babu yake aliyekuwa katika jeshi la kikoloni la K.A.R au maarufu kama Keya kwa wazee wa Afrika Mashariki na baba yake mzazi alivyokwenda Marekani masomoni.
Alichukua muda mrefu katika hotuba hii kuzungumzia mapambano dhidi ya rushwa na kusema kuwa Kenya na mataifa mengine ya Afrika lazima yatoe kiupaumbele katika kupambana na rushwa. Alisema rushwa ni kama "nanga ambayo inadidimza taifa chini."
Alitumia muda pia kuzungumzia umuhimu wa kushirikisha wanawake na wasichana katika maendeleo ya taifa. "Kama nusu ya timu haichezi, huwezi kushinda," alisema, akimaanisha kuwa nusu na huenda zaidi ya nusu ya wananchi wa Kenya ni wanawake, na kama hawapati fursa ya kushiriki kikamlifu katika elimu na shughuli nyingine za kijamii taifa la Kenya haliwezi kwenda mbele.