Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Novemba 05, 2024 Local time: 17:43

Obama, Kenyatta Wafungua Mkutano wa Ujasiriamali


Marais Barack Obama, wa Marekani na Uhuru Kenyatta, wa Kenya, wamefungua mkutano mkuu wa ujasiriamali - GES 2015 - mjini Nairobi Jumamosi, kwa wito wa vijana kubuni mbinu mpya za biashara na maendeleo na serikali kuuunga mkono juhudi hizo za vijana.

Akizungumza kwanza Rais Kenyatta, alisema vijana wa Afrika wako tayari na wana ubunifu wa kutosha na wakati umefika kwa serikali na makampuni binafsi kuhakikisha kwamba vijana wanapatia fursa kutekeleza ubunifu wao.

"Afrika iko mbioni," alisema Rais Kenyatta, na kuongeza kuwa Kenya imekaa tayari kabisa katika eneo la Afrika kwa kutekeleza ubunifu kama ilivyoonekana kwenye huduma ya kutuma fedha kwa simu M-Pesa ambayo ilianzishwa Kenya na sasa inatumiwa sehemu nyingi barani Afrika.

Rais Obama alisema Marekani inaongeza kiwango ilichotenga kwa ajili ya ujasiriamali kufikia zaidi ya dolla billioni moja kwa ajili ya kugharamia ubunifu wa vijana katika maeneo mbali mbali duniani.

Rais Obama alisema Marekani inafungua vituo vinne katika nchi za Zambia, Kenya na Mali kusaidia ubunifu unaofanywa na vijana wanawake kama njia ya kuhakikisha kuwa wanawake wanapatia fursa.

Alisema "kama nusu ya timu haiko uwanjani huwezi kushinda," na kuendelea kusema kuwa kwa nchi nyingi za Afrika nusu ya timu ni wanawake katika jamii.

Mamia ya vijana kutoka nchi mbali mbali duniani hasa barani Afrika wanahudhuria mkutano huu na kuzungumzia ubunifu wao huku wakijaribu kujiunganisha na makampuni au watu binafsi wanaoweza kufadhili miradi yao mipya.

Rais Obama, yuko nchini Kenya - nchi alikozaliwa baba yake - kwa mara ya kwanza kama rais wa Marekani.

Baadaye Jumamosi atazuru eneo la ubalozi wa Marekani wa zamani mjini Nairobi na kuweka shada la maua kukumbuka mamia ya watu waliouawa katika shambulizi la kigaidi la ubalozi huo mwaka 1998.

XS
SM
MD
LG