Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 10:43

Mwendesha Mashtaka wa ICC aahidi kuwasaidia waathirika wa machafuko DRC


Karim Khan
Karim Khan

Mwendesha mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) Karim Khan yuko Nchini DRC ambako ameahidi kujihusisha zaidi katika suala la kupatikana haki kwa waathirika wa machafuko na  manyanyaso ya ngono na ubakaji Mashariki mwa Congo.

Mwendesha mashtaka mkuu wa ICC aliyasema hayo wakati wa ziara yake mjini Bukavu ambako alikutana na Dr. Denis Mukwege ambaye anamiliki hospitali ya Panzi ambayo inawahudumia waathirika wa manyanyaso ya ngono mjini Bukavu. Dr. Mukwege pia na mshindi wa tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 2018.

Miongoni mwa watu waliomsubiri kwa hamu kubwa Karim Khan ni baadhi ya waathirika wa mauaji mbalimbali, ubakaji na hali tofauti za uhalifu waliotendewa katika baadhi ya vijiji vya jimbo la Kivu Kusini kabla kuundwa mahakama ya Kimataifa ya uhalifu ICC mwaka 2002.

Waathirika hao walitoka katika vijiji vya Makobola, Kasika, Katogota na pia mauaji yaliyofanyika Kaniola, Ninja, Mutarule na kadhalika, baada ya kuundwa kwa ICC.

Akiwa hana miguu tangu mwaka 1998, Bwami Samuel ametoka katika kijiji cha Kasika alifika kukutana na mwendesha mashtaka Mkuu wa ICC.

Bwami Samuel, anasema nimekuwa mlemavu kutokana na vita vilivyofanyika Kivu Kusini. Mwanasheria huyu tunamsihi kwamba waturudishie haki yetu ya awali na atusaidie kwamba wahalifu wasikilizwe na pia tunaomba msaada.

Mwendesha mashtaka mkuu wa ICC amesema amefanya ziara nchini Congo kwa mwaliko wa Rais Félix Tshisekedi katika lengo lake la kupambana dhidi ya kutoadhibiwa kwa watenda maovu.

Khan alikuwa amefuatana na waziri wa sheria Rose Mutombo, waziri wa haki za binadamu Fabrice Puela, Mwendesha mashtaka Mkuu wa Congo Firmin Mambu, Mkuu wa mahakama ya kijeshi jenerali Likulia Bakumi na mshauri wa rais Tshisekedi katika masuala ya uhusiano kati ya Congo na ICC, profesa Taylor Lubanga.

Khan amewahakikishia waathirika wa machafuko ya kivita mashariki mwa Congo kwamba atajihusisha binafsi kuhusu suala hilo, ila anataka ushirikiano zaidi kati ya serikali ya Congo na ICC, akijizuia kusema wazi ikiwa kuna uchunguzi mpya au uwezekano wa mashtaka mapya dhidi ya wababe wa kivita mashariki mwa DRC au la.

"Ni wakati wa kufanya kazi pamoja ili watoto hawa ambao nimewaona hivi punde, ambao walizaliwa na mabinti wenye umri mdogo pia, wawe kizazi cha mwisho kupitia kile mlichopitia. Ni rahisi kuzungumza-zungumza, na tumekuwa tukizungumza juu ya hili tangu 2004. Nadhani wakati umepita wa maneno-maneno. lazima tuchukue hatua na kufanya kazi pamoja, kwa ajili ya watu wa DRC, na watoto wenu”.

Akiwa ametoka Goma kumsikiliza Khan, Espoir Lukoo ni katibu mkuu wa shirika la utetezi wa haki za binadamu la SOPROP linalotetea mshikamano wa kijamii na amani Kivu Kaskazini, anasema, jimbo lao la Kivu Kaskazini kuna waasi wa M23 wanaozorotesha hali ya usalama. Wanataka hao nao pia waadhibiwe.

Kwa vile Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu haiwezi kufuatilia makosa kabla ya kuundwa kwake mnamo mwaka 2002, Daktari Denis Mukwege na mashirika kadhaa ya utetezi wa haki za binadamu wanataka iundwe mahakama maalum au vyombo vya sheria vya pamoja kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na ICC vinayoweza kufuatilia uhalifu wa zamani na kutoa adhabu kwa watakao patikana na hatia.

Karim Khan amekwenda mjini Bunia katika Jimbo la Ituri, kabla ya kukutana na Rais Tshisekedi mjini Kinshasa.

Mitima Delachance, Sauti ya America, Bukavu

Forum

XS
SM
MD
LG