Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) imefafanua kuwepo kwa vipindi vya mvua kubwa vitakavyo ambatana na upepo mkali na mawimbi makubwa.
Katika taarifa yake TMA imetoa tahadhari kuwa, kuanzia Jumamosi hadi keshokutwa kutakuwa na vipindi vifupi vya mvua kubwa inayozidi milimita 50 ndani ya saa 24.
Taarifa hiyo imesema mvua hizo zitaambatana na upepo mkali unaozidi kilomita 40 kwa saa na mawimbi makubwa yanayozidi mita mbili.
Kwa mujibu wa mamlaka hiyo mikoa inayotarajiwa kuathirika ni Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Lindi na Mtwara pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.
“Hali hii inatokana na kuimarika kwa ukanda wa mvua nchini na kuimarika kwa mgandamizo mkubwa wa hewa katika Bahari ya Hindi eneo la kisiwa cha Madagascar, hivyo kusababisha upepo mkali katika pwani ya Tanzania,” imesema taarifa hiyo.
TMA imewataka wakazi wa maeneo hayo kuchukua tahadhari na hatua stahiki na kwamba, inaendelea kufuatilia hali hiyo na itatoa mrejesho kila itakapobidi.