Mmiliki wa shule hiyo na mwalimu mkuu msaidizi walipandishwa kizimbani Ijumaa kwa makosa kadhaa ya usalama barabarani, ikiwa ni pamoja na kusafirisha watoto bila ya kuwa na vibali.
Katika ajali hiyo watu 35 walipoteza maisha wakiwemo wanafunzi wa darasa la saba, walimu na dereva wa gari la shule ya msingi iitwayo Lucky Vincent ya Arusha. Basi hilo lilikuwa limebeba waalimuna dereva, msaidizi wake na wanafunzi 27. Ajali hiyo ilitokea baada ya basi la shule kutumbukia katika korongo refu la mto Marera wilayani Karatu.
Wakisomewa mashitaka yao jana mbele ya Hakimu Mkazi wa Hakimu Mkazi Arusha, Desdery Kamugisha, Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Rose Sule alidai watuhumiwa hao wawili wamefunguliwa kesi Namba 78/2017 huku Mkurugenzi wa shule hiyo akishitakiwa kwa makosa manne na Mwalimu Nkana akishitakiwa kwa kosa moja.
Kwa mujibu wa gazeti la Habari Leo nchini Tanzania wakati Mkurugenzi wa Lucky Vincent akisomewa makosa yake, wakili huyo alidai kosa la kwanza ni la kuendesha gari la abiria bila ya kuwa na leseni ya usafirishaji ambapo Mei 6 mwaka huu katika eneo la Kwamrombo, Arusha Mjini akiwa mmiliki wa gari namba T 871 BYS aina ya Toyota Rosa, alifanya shughuli ya usafirishaji bila ya kuwa na leseni ya abiria.
Kosa la pili ni kuruhusu kuendesha gari bila ya kuwa na bima (Road Licence), Mei 6 mwaka huu akiwa mmiliki wa gari hilo aliruhusu gari hilo kuendeshwa bila ya kuwa na bima. Kosa la tatu ni kushindwa kuingia mkataba na mwajiriwa wake, Dismas Gasper ambapo Mei 6, 2017 akiwa mmiliki wa gari alishindwa kuingia mkataba na dereva huyo aliyeendesha gari lililopata ajali ambaye naye alifariki dunia katika tukio hilo.
Kosa la nne ni kubeba abiria zaidi ya 13 ambapo Mei 6 mwaka huu, mkurugenzi huyo ambaye ni Ofisa Msafirishaji na mmiliki wa shule ya Lucky Vincent alibeba na kusafirisha abiria zaidi ya 13 katika gari hilo kitendo ambacho ni kinyume na sheria.
Kosa la tano ni la Mwalimu Mkuu Msaidizi ambapo anashitakiwa kwa kuandaa safari iliyozidi abiria 13 ambapo ni kinyume cha sheria inadaiwa kuwa Mei 6 mwaka huu, Nkana akiwa Mwalimu Mkuu Msaidizi na mwandaaji wa safari alipakia abiria zaidi ya 13 kwenye gari lililosababisha vifo vya wanafunzi hao.
Baada ya washitakiwa hao kusomewa mashitaka yao yanayowakabili wakili anayewatetea washitakiwa hao, Method Komomogolo aliomba dhamana kwa washitakiwa hao huku Wakili wa Serikali Sule akisema hana pingamizi na dhamana yao.
Hakimu Kamugisha alitoa masharti ya dhamana kwa washitakiwa hao ambayo ni kila mshitakiwa alitakiwa kuwa na wadhamini wawili wawili watakaosaini bondi ya Sh milioni 15 na kwamba hawatakiwi kuondoka nchini au ndani ya mkoa bila ruhusa ya mahakama pamoja na kuwasilisha hati zao za kusafiria.
Watuhumiwa hao walitimiza masharti ya dhamana yao na kesi yao kuahirishwa hadi Juni 8, mwaka huu.