Kinakuwa ndicho kisa cha kwanza cha virusi vya polio barani Afrika, kwa kipindi cha zaidi ya miaka mitano, Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema.
Shirika hilo limesema katika taarifa yake kwamba utafiti wa kimaabara ulionyesha aina ya virusi vilivyogunduliwa nchini Malawi vina uhusiano na vile ambavyo vimekuwa vikisambaa nchini Pakistani, ambako ugonjwa huo unaathiri watu wengi.
Mpango wa Kimataifa wa Kutokomeza Polio ulisema kisa hicho, katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika, kilikuwa cha msichana mwenye umri wa miaka mitatu, ambaye alipata ugonjwa wa kupooza mwezi Novemba mwaka jana.
Kisa cha mwisho cha virusi vya polio barani Afrika kilitambuliwa kaskazini mwa Nigeria mnamo mwaka wa 2016 na duniani kote kulikuwa na visa vitano tu hapo mwaka jana.
Polio ni ugonjwa unaoambukiza kwa urahisi, ambao huvamia mfumo wa neva na unaweza kusababisha kupooza kabisa ndani ya saa chache. Ingawa hakuna tiba ya polio, ugonjwa huo unaweza kuzuiwa kwa kutumia chanjo, WHO ilisema.