Kwa mujibu wa shirika la habari la AP, mke wa Kony pamoja na watoto hao walirejeshwa Uganda Jumatano kwa ndege, wakiwa wanafamilia wa karibu zaidi kurejeshwa nchini, alisema Meja Jenerali Felix Kulayigye, ambaye ni msemaji wa jeshi. Kulayigye aliongeza kusema kwamba inaaminika kwamba Kony amejificha huko Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Kony ni kiongozi wa kundi la uasi linalopinga serikali ya Uganda la Lord’s Resistance Army au LRA, na ambalo linafahamika kwa kuteka nyara watoto na kisha kuwalazimisha kupigana. LRA lilianza miaka ya 80 na wakati lilipokuwa kwenye kilele cha nguvu yake, lilifahamika kutokana na ukatili wake dhidi ya raia nchini Uganda, Congo, Jamhuri ya Afrika ya Kati pamoja Sudan Kusini.
Kony anasakwa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai akikabiliwa na kesi 36 za uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu kaskazini mwa Uganda kati ya Julai 2002 na Desemba 2005. Kesi hizo zimepangwa kuanza kusikilizwa Septemba 9, wakati Marekani ikiahidi dola milioni 5 kwa yeyote atakayetoa taarifa zitakazopelekea kukamatwa kwake.
Mwaka 2012, kundi la uanaharakati lenye makao yake Marekani la Invisible Children, lilionyesha video kwenye mitandao ya kijamii ikiangazia ukatili uliyotekelezwa na LRA. Hata hivyo umaarufu wa kundi hilo umeshuka katika miaka ya karibu kufuatia kuuwawa au kukamatwa kwa makamanda wake wa ngazi za juu.
Forum