Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Novemba 24, 2024 Local time: 20:56

Mgomo: Serikali ya Kenya yafikia makubaliano na walimu


Wanafunzi wakitumia meza ya mwalimu darasani kujisomea wakati wa mgomo wa walimu wa nchi nzima wakidai nyongeza ya mshahara na hivyo kusimamisha masomo mjini Nairobi June 25, 2013. REUTERS/Noor Khamis
Wanafunzi wakitumia meza ya mwalimu darasani kujisomea wakati wa mgomo wa walimu wa nchi nzima wakidai nyongeza ya mshahara na hivyo kusimamisha masomo mjini Nairobi June 25, 2013. REUTERS/Noor Khamis

Serikali ya Kenya imesema imefikia makubaliano na waalimu nchini humo kusitisha mgomo ulioitishwa unaotishia kuvuruga shughuli za masomo hasa wakati wanafunzi wakijitayarisha kufanya mitihani ya kitaifa kuanzia Machi tarehe 7.

Chama cha kitaifa cha waalimu wa shule za sekondari na vyuo, KUPPET, kimesema kuwa kimekubali kufanya hivyo kwa maslahi ya wanafunzi wanaofanya mitihani ya kitaifa na kusisitiza kuwa kitatekeleza ilani ya mgomo baada ya mitihani hiyo kukamilika.

Waalimu hao wanataka serikali kupitia tume ya kuwaajiri walimu, TSC, kuanza mazungumzo kuhusu mkataba wa maelewano wa 2021-2025 unaowapa nyongeza ya mishahara kwa asilimia 70%.

Waziri wa Elimu Professa George Magoha ameeleza kuwa mazungumzo kati ya serikali na walimu hao chini ya muungano huo wa KUPPET yamejikita kwenye maslahi ya wanafunzi wanaoanza mitihani ya kitaifa, iliyocheleweshwa kutokana na maambukizi ya virusi vya Corona vilivyosababisha kalenda ya masomo kusitishwa.

“Kama kiongozi wa sekta hii ya elimu nimewashawishi wenzetu wasitishe mgomo lakini nieleze kama mwananchi kwa maoni yangu hakuna mtu isipokuwa Rais anayeweza kusimamisha mitihani hii,” amesema Waziri wa Elimu.

Walimu wa shule za sekondari na vyuo chini ya muungano wa KUPPET wamejikuta katika mzozo na serikali kupitia tume ya kuwaajiri walimu, TSC, kutokana na kile walimu wanachokitaja kuwa ni kucheleweshwa kwa mazungumzo ya pande mbili yanayohusu mkataba wa maelewano wa 2021-2025 unaowahakikishia nyongeza ya mishahara kwa asilimia 70% kutoka asilimia 30% wanayopokea sasa.

Lakini kutekelezwa kwa ilani ya siku saba ya mgomo wakati wanafunzi wa shule za msingi wanafanya mitihani ya KCPE kati ya Machi tarehe 7 na tarehe 10, huku wanafunzi wa kidato cha nne wakifanya mitihani ya KCSE kuanzia Machi tarehe 11, kumeshtumiwa na serikali.

Akello Misori, Katibu Mkuu wa KUPPET ameieleza VOA kuwa wamefikia uamuzi huo kuondoa tishio la kusambaratisha mitihani ya kitaifa, lakini kwamba punde tu wanafunzi watakapomaliza kufanya mitihani hiyo, walimu wataendelea na juhudi zao za kuitaka serikali, kupitia TSC kuweka saini mapendekezo yao ya mkataba mpya.

KUPPET katika mapendekezo yake inataka walimu kulipwa marupurupu yaliyoongezeka kutoka shilingi elfu 5,000 hadi 8,000 na walimu wa kiwango cha chini kulipwa shilingi elfu 20,800 kutoka shilingi 16,000 zinazolipwa katika mkataba wa sasa.

Katibu Mkuu Misori amesisitiza kuwa walimu wana haki ya kudai kulipwa mishahara minono chini ya mkataba mpya waliopendekezea TSC.

Awali, Nicholas Maiyo, ambaye ni mwenyekiti wa chama cha wazazi aliieleza VOA kuwa si haki walimu kuanza mchakato huo kuvuruga mitihani ya kitaifa wakati wazazi wameathirika zaidi na kalenda ya masomo iliyosogezwa pamoja kutokana na maambukizi ya virusi vya Corona.

Imetayarishwa na mwandishi wetu Kennedy Wandera, Nairobi, Kenya

XS
SM
MD
LG