Akizungumza wakati wa ziara yake huko Australia, McCain ameliambia Shirika la Utangazaji la Australia kuwa Russia imejaribu “kuangamiza misingi ile ile ya kidemokrasia” katika juhudi zake za kuingilia uchaguzi wa urais na chaguzi nyingine sehemu nyingine duniani.
Maoni hayo yamekuja wakati uongozi wa Rais wa Marekani Donald Trump ukikabiliwa na uchunguzi iwapo walikuwa na mafungamano na Russia, zikiwepo repoti kuwa Jared Kushner, mkwe wake na mshauri wa ikulu ya White House, alijaribu kuweka mfumo wa mawasiliano usio rasmi na maafisa wa Russia wiki chache kabla ya Trump kuapishwa.
“Najua kuwa baadhi ya maafisa wa serikali wanasema, “Sawa, huo ni utaratibu wa kawaida,” McCain amesema Jumatatu.
“Sifikirii huo ni utaratibu wa kawaida kufanyika kabla ya kuapishwa rais wa Marekani kwa mtu ambaye bado alikuwa hajapewa wadhifa katika serikali.
Gazeti la New York Times limemnukuu msemaji wa ikulu ya White House Hope Hicks akisema Kushner “ alikuwa anatekeleza hilo katika wadhifa wake kama afisa wa uongozi wa mpito,” na amekubali kuzungumzia mikutano hiyo na wabunge wanaochunguza suala hilo.
Trump ametupilia mbali madai yote kuhusu kampeni yake kushirikiana na Russia kuhujumu uchaguzi.
“Jared anafanya kazi nzuri kwa ajili ya nchi yake,” Trump ameliambia gazeti la Times Jioni Jumapili. “Nina imani naye.”
Anaheshimiwa na karibuni kila mtu na anashughulikia mpango utakao okoa mabilioni ya dola za nchi yetu. Aidha pamoja na hilo na pengine muhimu zaidi, ni mtu mzuri sana.
Kushner ambaye ana umri wa miaka 36, ambaye alikuwa ni mkurugenzi wa biashara ya majumba New York kabla ya kujiunga na wafanyakazi wa Trump wa ikulu ya White House, ni mume wa mtoto wa kwanza wa Trump Ivanka, ambaye pia ni mshauri wa ikulu ya White House.