Naibu msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Vedant Patel ameambia wanahabari kwamba “ Kufikia sasa hatujafanya tathmini yoyote inayoashiria kuwa Israel imevunja sheria za Marekani.” Marekani Oktoba 13 iliambia Israel kwamba ilikuwa na muda mwa mwezi mmoja wa kuongeza upelekaji wa misaada huko Gaza ambako miezi 13 ya vita kati ya Israel na kundi la Hamas vimesababisha janga la kibinadamu.
Iwapo Israel haingefanya hivyo kufikia Jumanne, basi Marekani ingepunguza upelekaji wa silaha kwake. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken Jumatatu alikutana na mshauri mkuu wa kiusalama wa kitaifa wa Israel Ron Dermer mjini Washington, ili kutathmini hatua zilizopigwa na Israel kuelekea upelekaji wa misaada huko Gaza.
Mjumbe wa Marekani kwenye UN Linda Thomas-Greenfield ameambia Baraza la Usalama la Umoja huo kwamba Israel imepiga hatua muhimu zikiwemo kurejesha upelekaji wa misaada kaskazini mwa Gaza, lakini ni lazima ihakikishe kuwa inatimiza majukumu yake yote kadri muda unavyokwenda.
Forum