Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 03:46

Marekani na Tanzania kuimarisha uhusiano wa biashara


Makamu wa rais wa Marekani Kamala Harris (kushoto) na mume wake Douglas Emhoff wakiwa wamewasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam Machi 29, 2023. Picha na ERICKY BONIPHACE/POOL/AFP.
Makamu wa rais wa Marekani Kamala Harris (kushoto) na mume wake Douglas Emhoff wakiwa wamewasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam Machi 29, 2023. Picha na ERICKY BONIPHACE/POOL/AFP.

Serikali ya Marekani imetangaza siku ya Alhamisi, mpango wa kuimarisha biashara na Tanzania, wakati Makamu wa Rais Kamala Harris anafanya ziara kama sehemu ya juhudi za kidiplomasia za Washington kuimarisa ushirikiano na bara la Afrika.

Harris alianzia ziara yake ya Afrika siku ya Jumapili huko Ghana, Jumatano jioni aliwasili katika mji mkuu wa kibiashara wa Tanzania Dar es Salaam, ambako anatarajiwa kufanya mazungumzo na Rais Samia Suluhu Hassan Alhamisi jioni.

Ofisi ya makamu wa rais ilitangaza mipango ya kuboresha biashara na masuala mengine yanayohusu mahusiano baina ya nchi hizo mbili, ikiwa ni pamoja na mkataba wa maelewano (MOU) kati ya Benki ya Export-Import ya Marekani (EXIM) na serikali ya Tanzania.

Hii itawezesha mpango wa mauzo ya nje ya bidhaa za Marekani zenye thamani ya dola milioni 500 ili kusaidia katika bidhaa na huduma katika sekta za miundombinu, usafirishaji, teknolojia ya digitali, hali ya hewa na usalama wa nishati na uzalishaji wa umeme.

Ofisi ya Harris pia imesisitiza msaada wa Marekani kwa mpango wa kufungua kiwanda kipya cha uzalishaji cha LifeZone Metals nchini Tanzania.

Kiwanda hicho ambacho kitatumia teknolojia ambayo haichafui mazingira, itazalisha nikeli na madini mengine yanayochimbwa katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki, kwa lengo la kuanza kusambaza kiwango cha betri za nikeli kwenda Marekani kuanzia mwaka 2026, ofisi ya Harris ilisema.

Kamala Harris anatarajiwa kuwepo Tanzania hadi siku ya Ijumaa na kuondoka kuelekea Zambia, ambako atakamilisha ziara yake.

Ziara yake Dar es Salaam inaashiria kurejea kwa ushirikiano wa kimataifa unaofanywa na Tanzania chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, baada ya kipindi cha kutengwa wakati wa utawala wa rais wa zamani wa Tanzania marehemu John Magufuli, ambaye alikatisha tamaa safari za nje ya nchi pamoja na kufuta safari zote za nje kwa mawaziri wake.

Chanzo cha habari hii ni shirika la habari la Reuters.

XS
SM
MD
LG