Harris alianza ziara yake ya bara la Afrika siku ya Jumapili nchini Ghana, na aliwasili Jumatano jioni katika mji mkuu wa kibiashara wa Tanzania, Dar es Salaam, ambako amefanya mazungumzo na Rais Samia Suluhu Hassan, na wawili hao kuhutubia waandishi wa habari.
Ziara ya Harris ya nchi tatu barani Afrika, inalenga kuimarisha uhusiano na bara la Afrika, ambako China na Russia zinazidi kuongeza ushawishi wao.
AHarris alitangaza mipango ya kuboresha biashara na masuala mengine ya mahusiano baina ya nchi hizo mbili, ikiwa ni pamoja na mkataba wa makubaliano (MOU) kati ya Benki ya Mauzo ya Nje ya Marekani (EXIM) na serikali ya Tanzania.
Mkataba huo unatarajiwa kurahisisha utoaji wa hadi dola milioni 500, kufadhili mchakato wa mauzo ya Marekani kwa Tanzania, na pia kusaidia mauzo ya bidhaa na huduma katika sekta mbalimbali zikiwemo miundombinu, uchukuzi, teknolojia ya kidijitali, usalama wa hali ya hewa na nishati, na uzalishaji wa umeme.
Harris pia amesema ziara hiyo inaangazia msaada wa Marekani kwa mpango wa LifeZone Metals wa kufungua kiwanda kipya cha usindikaji nchini Tanzania.