Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Novemba 22, 2024 Local time: 01:35

Tanzania yaombwa kuweka mikakati ya kujifunza Kiswahili


Wanafunzi wa shule ya Al-Nour wakiwa darasani huko Zanzibar. Picha na REUTERS/Thomas Mukoya.
Wanafunzi wa shule ya Al-Nour wakiwa darasani huko Zanzibar. Picha na REUTERS/Thomas Mukoya.

Wasomi na wadau wa Kiswahili nchini Tanzania wanasema mamlaka zinapaswa kuweka mkakati maalum wa kutumia Kiswahili katika nyanja zote za kiuchumi na kielimu ili kuboresha maarifa ya wananchi kwa kuwafundisha kwa lugha wanayoielewa.

Aidha, wanasema ni vyema vitabu vikaandikwa kwa Kiswahili halisi kinachotumiwa na watu wa kawaida badala ya kutumia Kiswahili sanifu pekee.

Lugha ya Kiswahili ambayo imekuwa ikikua ndani na nje ya bara la Afrika. ni lugha inayozungumzwa na zaidi ya watu milioni 230 katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, huku ikiwa miongoni mwa lugha zinazotumiwa katika Umoja wa Afrika.

Prof. Katrina Thompson wa Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison Marekani amesema wanafunzi wengi hujifunza Kiswahili sanifu cha vitabu na kuwafanya kushindwa kuzungumza vizuri wanapofika Afrika Mashariki.

Hivyo ameshauri vitabu viandikwe pande zote ili kuwawezesha wageni kuzungumza Kiswahili kwa urahisi.

“Ingekuwa vizuri kama vitabu vinaonyesha kiswahili halisi kinavyotumiwa sio sanifu tu ambacho labda ni kiswahili cha Habari na magazeti lakini sio kiswahili kinacho tumiwa na watu wa kawaida yaani ni vizuri kujua viswahili mbalimbali cha kitabu na chamtaani pia” amesema.

Wasomi wanasema kuwa kiswahili ni jukwaa muhimu la mawasiliano na utamaduni katika Afrika Mashariki na Kati, na linachangia katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Kueneza matumizi yake katika maisha ya kila siku kunaweza kuimarisha uwezo wa jamii kujitegemea kielimu na kiuchumi.

Dkt. Seleman Sewanji, mdau wa Kiswahili amesisitiza umuhimu wa kuweka mkakati maalumu wa kutumia Kiswahili hasa katika elimu, kwa lengo la kuimarisha uchumi na maarifa ya jamii. Huku akiamini kuwa ufahamu mzuri wa lugha ni msingi muhimu wa kupata maarifa.

Mwalimu akifundisha wanafunzi katika shule iliyopo hifadhi ya Taifa ya Singita Grumeti, Tanzania. Picha na REUTERS/Baz Ratner.
Mwalimu akifundisha wanafunzi katika shule iliyopo hifadhi ya Taifa ya Singita Grumeti, Tanzania. Picha na REUTERS/Baz Ratner.

Amesema “Wenye mamlaka waweke mkakati maalum wa kutumia Kiswahili. Kiswahili kinatunufaishaje kiuchumi na kielimu?” na kuongeza kuwa “Huwezi kuwa na uchumi bora kama watu wako hawana maarifa mazuri, na maarifa mazuri yanapatikana pale watu wanapofundishwa kitu kwa kuelewa vizuri. Ukishaweka mkakati huo, tutajua sasa tufanye nini kwa lugha.”

Hata hivyo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKIZA), Dkt. Mwanahija Ali Juma, amesema hata kama patakuwepo na sera ya lugha kati ya Tanzania na Zanzibar, endapo sera ya elimu haitoeleza kuwa Kiswahili ndio kitumike kufundishia, bado itakuwa ngumu kukikuza Kiswahili.

“Lakini hata kama tutapewa sera ya lugha ikiwa sera ya elimu itakuwa haikuanisha kuwa lugha ya kufundishia iwe lugha ya kiswahili itakuwa ni sawasawa na sifuri kwasababu sera ya elimu ndio inaongoza mitaala ya kufundishia katika sikuli mbalimbali” amesema Juma .

Dkt. Juma amemalizia kwa kuwataka viongozi kuwa na utashi wa kutoa ushauri bungeni na katika baraza la wawakilishi ili kutengeneza sera ya elimu itakayotamka moja kwa moja Kiswahili kuwa lugha ya kufundishia shuleni.

Imetayarishwa na Amri Ramadhani Sauti ya Amerika Dar es Salaam.

Forum

XS
SM
MD
LG