Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Januari 07, 2025 Local time: 05:47

Rais wa Guinea Bissau yupo nchini Tanzania kwa ziara ya kiserikali


Rais wa Guinea Bissau Umaro Sissici Embalo (L) na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan
Rais wa Guinea Bissau Umaro Sissici Embalo (L) na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan

Nchi hizi mbili zimekubaliana kushirikiana katika kilimo cha korosho, Uchumi wa Bluu, utalii

Rais wa Guinea Bissau, Umaro Sissoco Embalo, yuko nchini Tanzania kwa ziara ya siku tatu, kupitia ziara hiyo wachumi wameihimiza serikali ya Tanzania kutumia fursa ya ushirikiano na Guinea Bissau kujifunza njia za kuongeza thamani ya zao la korosho. Lengo ni kuhakikisha wakulima wa korosho wanapata faida zaidi.

Wachumi pia wamependekeza wataalamu mbalimbali wahusishwe katika mazungumzo ya makubaliano kati ya nchi hizo mbili ili kuhakikisha kuwa masuala yanayojadiliwa yanatekelezwa kikamilifu.

Nchi ya Guinea Bissau ni miongoni mwa nchi iliyofanikiwa katika ulimaji na uzalishaji wa zao la korosho ambapo thamani ya uuzaji wa zao hilo nje ya nchi inafikia takribani asilimia 90 na kuchangia kwa asilimia 80 kama chanzo kikuu cha mapato ya wakulima wadogo huku zao hilo likichangia asilimia 10 ya pato la taifa la nchi ya Guinea Bissau.

Suala ambalo Dkt Eliaza Mkuna Mhadhiri Mwandamizi wa Uchumi, Chuo Kikuu cha Mzumbe, Morogoro anasema ni wakati wa Tanzania kutumia fursa ya ushirikiano baina ya Tanzania na Guinea Bissau kujifunza namna gani wanaweza kufanya kuhakikisha kwamba zao la korosho linawafaidisha Watanzania.

“Pengine ni wakati sasa wakuona taasisi kama bodi ya korosho inawezaje kashirikiana na taasisi ambazo zipo katika nchi ya Guinea Bissau kuona ni namna gani ambayo wao wameweza kufikia hatua ya mbali ya kuona zao la korosho linawafaidisha” amesema Mkuna.

Viongozi wakishuhudia utiaji saini mkataba katika sekta ya uwekezaji na biashara
Viongozi wakishuhudia utiaji saini mkataba katika sekta ya uwekezaji na biashara

Kufuatia ziara hiyo Tanzania na Guinea Bissau zimekubaliana kushirikiana katika maeneo mbalimbali ikiwemo kilimo cha zao la korosho, Uchumi wa Bluu ukihusisha Uvuvi, utalii, fukwe na usafirishaji baharini, Ulinzi na usalama vilevile nchi hizo mbili zimesaini mkataba wa makubaliano wa ushirikiano katika sekta ya uwekezaji na Biashara.

Akizungumza na waandishi wa habari Rais Samia Suluhu Hassan ameeleza kuwa kutokana na Tanzania na Guinea Bissau kuwa wazalishaji wakubwa wa zao la korosho makubaliano yao yanatarajia kuanzia katika kufanya tafiti na kuongeza thamani ya zao la korosho katika mataifa hayo mawili.

“Kama mnavyojua kwamba nchi zetu mbili Guinea Bissau na Tanzania ni wazalishaji wakubwa na wazuri wa zao la korosho kwahiyo hilo ndio eneo ambalo tumesema tuanze ushirikiano hasa kwenye kufanya tafiti na kuongeza thamani ya mazao yetu” Amesema Rais Samia.

Rais wa Guinea Bissau Umaro Sissici Embalo (L) akiwa na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.
Rais wa Guinea Bissau Umaro Sissici Embalo (L) akiwa na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza na Sauti ya Amerika Prof Omar Fakih kutoka Zanzibar anasema ili kuhakikisha makubaliano yanayofanyika yanakuwa na tija ni muhimu kwa serikali kuhusisha wataalamu wa sekta mbalimbali ili waweze kupendekeza makubaliano ambayo yanatekelezeka.

“Kuna mambo mengine yangeanza na wataalamu wa chini au waandamizi ambao wapo kwenye sekta fulani wamgeachiwa kufanya makubaliano kabla ya viongozi wa kisiasa ili waweze kupendekeza mambo ambayo yanaweza kutekelezeka” Amesema Prof Fakih

Nae Rais Umaro Sissoco Embalo akihitimisha amewakaribisha Watanzania ambao wanafanya kazi katika sekta binafsi nchini Guinea Bissau kuangalia fursa za kibiashara na za kiuchumi zilizopo nchini humo kwakuwa nchi hiyo inaweza kuwa kiunganishi kizuri kati ya Tanzania na nchi za Afrika ya Magharibi.

Imeandaliwa na Amri Ramadhani Sauti ya Amerika.

Forum

XS
SM
MD
LG