Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 07:11

Makonda avuliwa ukuu wa mkoa wa Dar es Salaam


Paul Makonda
Paul Makonda

Rais wa Tanzania John Magufuli Jumatano amemuondoa Paul Makonda katika wadhifa wake kama mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam ambaye ametumikia nafasi hiyo tangu rais aingie madarakani.

Huenda hatua ya kuondolewa kwake ni kwa sababu ametangaza nia ya kugombea nafasi ya ubunge katika jimbo la Kigamboni, Dar es Salaam.

Makonda amekuwa ni mwenye utatanishi mkubwa tangu alipoingia katika wadhifa huo.

Miongoni mwa masuala yenye utatanishi ni pale alipotangaza watu wanaofanya mapenzi ya jinsia moja wakamatwe jambo lililokemewa na makundi ya haki za binadamu na mataifa mbalimbali duniani.

Mwezi Januari 2020 Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilimpiga marufuku yeye na mkewe Mary Felix kuingia Marekani.

Kupigwa marufuku huko kulitokana na shutuma ya kuwa Makonda anashiriki katika ukandamizaji wa haki za binadamu ikiwa ni pamoja na kunyima watu haki ya kuishi, haki ya uhuru wa kujiamulia mambo na usalama wa watu. Pia huenda suala la kampeni ya kuwakamata mashoga ikawa ni moja ya sababu hizo.

Hata hivyo Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania ilimkana Mkuu wa Mkoa huyo katika kampeni yake ya kuwakamata na kuwashtaki mashoga katika tamko la serikali la Novemba 4, na ikadai kuwa kampeni hiyo ni mawazo binafsi ya Makonda na si msimamo rasmi wa serikali.

Pia shutuma nyingine ni kwa kiongozi huyo kutumia nafasi yake hiyo, kukandamiza upinzani wa kisiasa, kukandamiza haki ya kujieleza, na kushambulia makundi yasiyo na sauti.

Lakini Makonda pia alianzisha kampeni kadhaa ambazo hazikuwa na hitimisho ikiwemo za wasanii dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya. Hata hivyo hakuna msanii aliyefikishwa mahakamani baada ya kamata kamata hiyo.

Kampeni nyingine iliyoanzishwa na Makonda ni ile ya tezi-dume ambapo alidai timu yake itapita nyumba hadi nyumba kuwapima kinababa.

Kadhalika Makonda alianzisha kampeni ya kuwafungulia mashtaka na kuwawajibisha wanaume wote wanao wanyanyasa wake zao au wapenzi wao.

XS
SM
MD
LG