Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 04:42

UN imeridhia Monusco kuendelea kulinda amani DRC


Balozi Augustine Mahiga
Balozi Augustine Mahiga

Baraza la usalama limepitisha kwa kauli moja azimio jipya kuhusu kuongeza muda kwa vikosi vya Umoja wa Mataifa vya kulinda amani (Monusco na intervention brigade force) kuwepo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Hata hivyo kwa kauli moja wanachama wote 15 wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa wamekubaliana kwamba Monusco pamoja na intervention brigade force lazima vipewe uwezo zaidi ili kupambana na hali mpya iliyojitokeza huko DRC.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Augustine Mahiga ambaye anaziwakilisha nchi za SADC amesema kuwa: “Tulikuwa tunataka tuhakikishe muda wa kikosi cha Monusco na hasa kile kikosi kinachoitwa intervention brigade force kinaongezewa muda.”

Ameeleza kuwa sababu kubwa kikosi cha Intervention brigade force ndio kinachofanya kazi kubwa ya kupambana na vile vikundi mbalimbali ambavyo vimekuwa vinaleta matatizo kwa usalama wa watu wa Kongo.

Mahiga amefafanua kuwa hivi sasa kuna mambo mapya makubwa matatu yamejitokeza. Kwanza kuna vikundi ambavyo vinajitokeza ambavyo havikuwepo huko nyuma na vitahitaji kazi kubwa kwa upande wa intervention brigade force.

Jambo la pili amesema kuna nafasi ya pekee ambayo haijawahi kutokea kwa kuwa na mkataba wa Amani uliotiwa saini kule Kongo tarehe 31 Disemba mwaka jana.

Amesema kuwa mkataba huu utaweza kuipeleka Kongo kwenye uchaguzi mwishoni mwa mwaka huu.

“Sasa hii ni nafasi ya pekee kwa kuongeza muda Monusco ili ishiriki katika kuhakikisha kwamba makubaliano hayo ya kisiasa yanafanikiwa,” amesema Mahiga.

Mahiga ameongeza kuwa jambo la tatu ni fursa ya kipekee katika kushughulika na vikundi mbalimbali ambavyo vimekuwa vinawanyanyasa, kuwaumiza na kuwaua raia sio tu katika mikoa mikubwa miwili ya Kivu, lakini sasa hivi tunashuhudia pia katika sehemu za Kasai na sehemu nyingine.

“Kwa hivyo kuna jukumu la pekee kuhusu Monusco kujipanga upya ikishirikiana na kikosi chake cha intervention brigade force kuweza kufanya kazi inayojulikana kwa sababu watu wengi walikuwa hawaridhiki na kazi iliyokuwa inafanywa katika kulinda raia,” amefafanua waziri huyo.

Ingawaje katika majadiliano kuhusu kuwepo vikosi hivyo Kongo, Marekani walikuwa wanafikiria kuwa majeshi hayo yapunguzwe.

Baraza hilo limesema kamwe "tusikubali nafasi hii ya kufanya uchaguzi kupotea na pia kuhakikisha mageuzi ya siasa yanaendelea vizuri."

Ingawa kuna baadhi ya wanachama wa baraza la usalama ambao wanadhani hii isiwe kitu cha kawaida kwa sababu Umoja wa Mataifa haupaswi kuingia vitani.

“Lakini hali ya Kongo sio hali ya kawaida na tunahitaji maamuzi ambayo sio ya kawaida ili kurekebisha hali ya Kongo,” amesema waziri huyo.

Mahiga anasema kuwa SADC imewahakikishia baraza la usalama kwamba itafanya kazi karibu na wakongo. Kwa mujibu wa Waziri mazungumzo hayo yamekwenda vizuri.

“Unaonekana mjadala huu ulikuwa mgumu, ulikuwa upigiwe kura siku tatu zilizopita lakini majadiliano yaliendelea…Hatimaye wanachama wote 15 wa baraza la usalama wamefikia mwafaka na wamenikaribisha mimi nizungumze kwa niaba ya nchi za SADC,” amesema waziri Mahiga.

Kikosi cha Monusco kilikuwa na matatizo na ndio maana na sisi nchi za SADC tulisema tunahitaji kikosi kingine ndani ya Monusco, amesema waziri.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Salehe Mwanamilongo, New York.

XS
SM
MD
LG