Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 23:49

Mahakama yaondoa ukomo wa umri kwa wagombea urais Uganda


Bunge la Uganda likijadili kubadilisha katiba kuongeza muda wa uongozi wa rais, Kampala, Uganda, Septemba 21, 2017.
Bunge la Uganda likijadili kubadilisha katiba kuongeza muda wa uongozi wa rais, Kampala, Uganda, Septemba 21, 2017.

Mahakama ya katiba Uganda imeidhinisha mabadiliko ya katiba yalioondoa ukomo wa umri kwa wagombea urais.

Mwandishi wa idhaa ya Kiswahili VOA anaripoti kuwa katika kikao cha mahakama mjini Mbale, mashariki mwa Uganda kilichochukuwa zaidi ya masaa 13, majaji wameamua kwamba kuweka kizuizi cha umri kwa wagombea urais, ni ubaguzi, na kwamba bunge halikuvunja sheria yoyote kwa kuifanyia mabadiliko katiba ya taifa.

Katika uamuzi wa majaji 4 dhidi ya 1, wakiongozwa na naibu wa Jaji Mkuu Alphonse Owing Dollo, mahakama imesema kwamba maana ya nchi ni Zaidi ya kundi la watu lenye hisia za uzalendo na kwamba bunge lilizingatia ibara ya 79 ya katiba, kuifanyia hiyo katiba mabadiliko na kuondoa umri kwa wagombea wa urais.

Msimamo wa Jaji Cheborion Barishaki

Jaji Cheborion Barishaki amefafanua kuwa kwa kutunga ibara ya 3 na 7, bunge lilifuata kanuni zote zinazohitajika kikatiba.

"Mswada ulikuwepo, maoni ya raia yalikusanywa, ulichapiswa kwa gazeti rasmi la serikali, ukasomwa kwa mara ya kwanza, ya pili na tatu. Ulipitia kwa kamati ya bunge, ukajadiliwa na kupitishwa. Mabadiliko ya sheria yalifanyika kulingana na sheria," ameeleza.

Ameongeza kuwa wabunge waliopitisha mabadiliko hayo ya kumruhusu rais kutawala bila ya kujali ukomo wa umri, wamepata pigo, baada ya hatua yao ya kutaka kujiongezea muda wa muhula wao kutoka miaka 5 hadi 7 kukataliwa na majaji wote 5.

"Mahakama, imeamua kwamba wabunge walionyesha ulafi kwa kukosa kuheshimu wapiga kura na badala yake kujiongezea mda wa kuwa bungeni bila kutafuta maamuzi ya wapiga kura baada ya mda wao wa miaka 5 kukamilika," amesema.

Msimamo wa Jaji Alphonse Owing Dollo

Kwa upande wake Jaji Alphonse Owing Dollo amesema kuwa hatua ya wabunge ilivunja mkataba wa kisheria kati yao na wapiga kura wa kuhudumu kwa muhula wa miaka 5.

"Wabunge walikaidi na kutenda Zaidi ya mamlaka walio nayo, na kunyakuwa madaraka ya raia kikatiba kwa kujiongezea mda wa kuhudumu bungeni ilivyo katika ibara ya 1 ya katiba, amesema.

Mabadiliko ya katiba

Majaji hao wamefutilia mbali mabadiliko ya ibara ya 2, 6 na 10 ya mabadiliko ya katiba ya mwaka 2017, ambayo pia iliongeza muda kwa viongozi wa serikali za mitaa kutoka miaka 5 hadi 7. Viongozi wa serikali za mitaa ndio waliotumiwa na chama kinachotawala cha NRM, kubadilisha katiba hiyo, kama wapiga kura ambao walitoa maoni yao, Disemba 2017.

Hatua hii inampa uhuru Rais Yoweri Museveni kuwania muhula mwingine tena na ana uhuru wa kuwania mihula mingine miwili zaidi ya miaka 5 kila mmoja.

Museveni,mwenye umri wa miaka 73, amekuwa madarakani tangia mwaka 1986.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Kennes Bwire, Washington, DC

.

XS
SM
MD
LG