Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Julai 01, 2024 Local time: 02:24

Mahakama ya juu ya Burundi yathibitisha kifungo cha maisha dhidi ya waziri mkuu wa zamani


Waziri mkuu wa zamani wa Burundi Alain Guillaume Bunyoni
Waziri mkuu wa zamani wa Burundi Alain Guillaume Bunyoni

Mahakama ya juu nchini Burundi Alhamisi ilithibitisha kifungo cha maisha dhidi ya waziri mkuu wa zamani wa nchi hiyo, Jenerali Alain Guillaume Bunyoni, chanzo cha mahakama kimeliambia shirika la habari la AFP.

Akiwa mmoja kati ya vigogo waliokuwa na ushawishi mkubwa katika utawala wa Burundi, Bunyoni alikuwa waziri mkuu kuanzia katikati ya mwaka 2020 hadi Septemba 2022, ambapo alifutwa kazi, siku chache baada ya Rais Evariste Ndayishimiye kuonya juu ya njama ya kumuondoa madarakani.

Alihukumiwa kifungo cha maisha jela mwezi Disemba mwaka jana kwa mashtaka kadhaa ikiwemo kutumia uchawi ili kudhuru maisha ya rais, kuhujumu uchumi na kujitajirisha kwa njia haramu.

“Emmanuel Gateretse, mkuu wa Mahakama ya juu amethibitisha uamuzi wa jaji wa kwanza dhidi ya Jenerali Bunyoni na kuongeza faini ya bilioni 22.7 pesa za Burundi pamoja na kutaifisha mara moja mali zake ambazo hakuzitangaza,” chanzo cha mahakama kimesema kwa masharti ya kutotajwa jina.

Katika kesi yake ya rufaa mwishoni mwa mwezi Mei, Jenerali Bunyoni alikanusha tena mashtaka yote dhidi yake na kuomba “aachiliwe huru”.

Tangu alipochukua madaraka mwezi Juni 2020, Ndayishimiye alipongezwa na Jumuia ya kimataifa kwa kumaliza hatua kwa hatua kutengwa kwa Burundi chini ya utawala wa Nkurunziza.

Forum

XS
SM
MD
LG