Mfanyabiashara huyo anatuhumiwa kuendesha biashara ya mabilioni ya pesa kwa minajili ya kukwepa vikwazo vya uchumi vilivyowekwa dhidi ya nchi ya Iran.
Zarrab ni mwenye kumiliki mamilioni ya fedha, umri miaka 33, mwenye uraia pacha wa Iran na Uturuki na ambaye anamaslahi ya kibiashara nchini Uturuki na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), na pia mafungamano na serikali ya Uturuki na Iran.
Mfanyabiashara huyu alikamatwa katika jimbo la Florida Machi 2016 akiwa katika ziara pamoja na familia yake kwenye eneo la starehe la Disney World na baadae kuhamishiwa New York.
Mfanyabiashara huyo anakabiliwa na tuhuma za jinai kwa kuisaidia Iran kukwepa vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa na Marekani kati ya mwaka 2010 na 2015 kwa kuzungusha fedha katika mifumo ya kifedha ya Marekani na kuwahonga maafisa wa Uturuki.
Kesi hiyo ambayo inasubiriwa kufanyika imekuwa ndiyo kiini cha kuendelea kuzorota kwa mahusiano kati ya Marekani na Uturuki.
Rais wa Uturuki Recept Tayyip Erdogan yeye binafsi amekuwa akijaribu kuibembeleza Marekani kumwachia Zarrab, ambapo maswali mengi yameibuka kuwa huenda Erdogan na maafisa wa Uturuki wanawasiwasi kuwa Zarrab anaweza kuwahusisha na tuhuma hizo za rushwa na ufisadi.