Umoja wa Falme za Kiarabu, mzalishaji mkuu wa mafuta, ni mwenyeji wa mkutano wa kilele wa mwaka huu, unaojulikana kama COP28. Mkutano huu unajiri huku wanasayansi wakuu wakitoa tahadhari kwa ulimwengu kuhusu kufikia malengo yake ya hali ya hewa.
Mkutano wa COP 28 unazileta pamoja karibu nchi 200 ambazo zilikubali Mkataba wa Mfumo wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya hali ya hewa ya mwaka 1992.
Wanadiplomasia kutoka mataifa hayo wamekuwa wakikutana kila mwaka tangu 1995. Hii ni mara ya 28 kwa mkutano huu kufanyika na hivyo kutambulika kama COP 28.
Rais Biden hatahudhuria mkutano wa kilele wa viongozi wa dunia Ijumaa na Jumamosi mwanzoni mwa COP28, kulingana na ratiba rasmi ya White House iliyotolewa Jumapili.
Haijulikani ikiwa Biden atasafiri hadi Dubai katika wiki ya pili ya mashauriano, wakati viongozi wengine wa ulimwengu baadhi yao watakuwa wameondoka .
Shirika la Afya Duniani (WHO) pamoja na jumuiya ya afya duniani, wanapaza sauti zao kuhakikisha kwamba athari za mabadiliko ya hali ya hewa kwa afya zinachukua nafasi kubwa katika mazungumzo hayo.
Maria Neira, Mkurugenzi wa Idara ya Hali ya Hewa, Mazingira, na Afya ya WHO, alisema, "Ni wakati muafaka kwa sekta ya afya kuchukua nafasi kuu katika masharuaino ya COP.
Kwa sababu ni dharura. Kwa sababu mabadiliko ya hali ya hewa yanaathiri vibaya sana afya zetu, na yanaathiri kwa sababu tuna matukio mabaya zaidi ya hali ya hewa, tuna watu wengi waliohamishwa,” alisema Neira na kuongeza kuwa
“tuna hewa yenye sumu kali na iliyochafuliwa. Tuna uhaba wa maji, uhaba wa chakula, magonjwa yanayoenezwa na wadudu, magonjwa yasiyo ya kuambukiza, maswala ya afya ya akili. Kila kitu kiko hatarini kwa sababu ya mabadiliko ya hali ya hewa.”
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anasema safari yake ya hivi majuzi huko Antarctica inasisitiza haja ya viongozi wa dunia katika mkutano wa COP 28 wa mazingira huko Dubai kushughulikia kwa haraka jinsi ya kupunguza ongezeko la joto duniani.
Antonio Guterres alisema “Viongozi lazima wachukue hatua kupunguza viwango vya joto duniani hadi digrii 1.5, wa watu kutokana na machafuko ya hali ya hewa, na kukabili gesi chafu. Tunahitaji dhamira ya kimataifa ya kutekeleza upya mara tatu, ufanisi wa nishati maradufu, na kuleta nishati safi kwa wote ifikapo 2030.”
Moja ya masuala magumu zaidi yanayokabili mazungumzo ya COP28 ni mustakabali wa nishati ya mafuta. Nchi zitajadili iwapo zitakubali kwa mara ya kwanza kusitisha matumizi ya makaa ya mawe, mafuta na gesi.
Takriban mataifa 80 yanaelekea kwenye COP28 yakiangazia makubaliano ya kusitisha nishati ya mafuta, ikiwa ni pamoja na Marekani, Umoja wa Ulaya na mataifa ya visiwa vidogo vinavyoathiriwa na hali ya hewa.
Hata hivyo, nchi nyingine zinapinga. G20 ilishindwa kuafikiana kuhusu suala hili katika mkutano wa mapema mwaka huu, na nchi ikiwa ni pamoja na Russia, zimesema hadharani zitapinga mpango huo.
Fedha ni suala kuu katika kila mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya hewa, na ni muhimu sana katika ajenda ya COP28 kwa sababu nchi zitajaribu kuzindua hazina mpya ya kukabili uharibifu wa hali ya hewa ili kuzisaidia nchi zilizo hatarini kwa gharama ambazo zinakabiliwa na athari za hali ya hewa
Masuala mengine ambayo nchi zitajadili katika COP28 ni pamoja na ahadi za kuongeza mara tatu nishati mbadala na ni jukumu gani teknolojia ya kupunguza kaboni inapaswa kuchukua katika kufikia malengo ya hali ya hewa.
Forum