Wakati huo huo wataalamu wanasisitiza elimu zaidi kuendelea kutolewa juu ya matumizi sahihi ya viwatilifu vya kilimo kwakuwa matumizi yasiyosahihi ni moja ya sababu ya kutoweka kwa vyakula hivyo.
Moja ya changamoto inayokumba jamii nyingi hivi sasa ni kutoweka kwa vyakula vya asili ambavyo vimekuwa chanzo muhimu cha lishe kwa vizazi vingi huku sababu moja wapo ya kutoweka huko ikiwa ni matumizi ya viwatilifu visivyofaa katika kilimo.
Matumizi hayo ya viwatilifu visivyofaa yanatokana na baadhi ya wakulima kutofahamu matumizi sahihi ya viwatilifu hivyo, kama anavyoeleza Mussa Chidinda Kaimu Meneja wa usimamizi wa Afya ya mimea kutoka Mamlaka ya Afya ya mimea na viwatilifu Tanzania.
Chidinda anaeleza: "Usipokuwa na taarifa sahihi za viwatilifu na uchaguzi wa viwatilifu basi unaambulia kupata nusu ya mazao au usipate kabisa kile ulichokusudia kwahiyo sisi tunafanya nini katika eneo hili kuchagiza uzalishaji sisi tunahakikisha kwamba viwatilifu vyote vinavyouzwa ndani ya nchi hii ni salama kwa kilimo cha nchi hii na ni salama kwa mzalishaji na mlaji akifuata mashariti ambayo tumempa."
Baadhi ya sababu zinazopelekea kutoweka kwa vyakula vya asili ni pamoja na mabadiliko ya tabia nchi yanayopelekea vyakula vya asili kushindwa kuhimili mabadiliko hayo pamoja na kilimo cha kisasa kinachohimiza matumizi ya mbegu za kisasa hali inayopelekea baadhi ya wakulima kuona mazao ya asili yamepitwa na wakati.
Diomedesi Kalisa kutoka Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) ameitaka jamii kuacha kuchukulia vyakula vya asili kupitwa na wakati na baadala yake wanapaswa kujifunza na kuelewa faida zinazopatikana kutokana na kula vyakula vya asili.
Kalisa anafafanua kuwa: "Watu wengi wanaweza wakawa wanadhani hivi vyakula vya asili vimepitwa na wakati wakiviangalia wanavidharau wanaona ni vyakula vya masikini lakini kumbe vinafaida kwahiyo watu wenyewe kwanza wanatakiwa kutambua faida zilizopo katika hivi vyakula vya asili nikichukulia mfano wa mahindi ya asili."
Hata hivyo Domina Jeremiah Afisa lishe kutoka Biharamulo ameitaka jamii kuendelea kujitokeza katika mafunzo mbalimbali yanayotolewa juu ya matumizi sahihi ya viwatilifu ili kuhakikisha vyakula asilia havitoweki.
Jeremiah anatoa ushauri: "Wito wangu kwa wananchi waendelee kuitikia kwa wingi wanaposikia kuna uelimishaji juu ya matumizi bora ya mbolea na viwatilifu matumizi ya mbolea asilia au matumizi sahihi ya mbolea wanazopewa na wataalamu ili tuweze kurejesha vyakula vyetu vya asili.
Kalisa amehitimisha akisisitiza umuhimu wa kulinda vyakula asilia na kuhimiza matumizi sahihi ya viwatilifu, akizingatia kauli mbiu ya mwaka huu inayosema “Haki ya chakula kwa wote, kwa maisha ya sasa na ya baadae.” Amesema hatua hizo ni muhimu ili kuhakikisha upatikanaji wa chakula salama na chenye ubora kwa kila mtu.
Imetayarishwa na mwandishi wetu Amri Ramadhani, Dar es Salaam, Tanzania.
Forum