Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Desemba 27, 2024 Local time: 07:23

Kibaki azikwa


Jeneza lililoubeba mwili wa aliyekuwa rais wa tatu wa Kenya, Mwai Kibaki.
Jeneza lililoubeba mwili wa aliyekuwa rais wa tatu wa Kenya, Mwai Kibaki.

Mwili wa aliyekuwa rais wa tatu wa Kenya, Mwai Kibaki, aliyeaga dunia Ijumaa wiki iliyopita, Jumamosi ulizikwa nyumbani kwake katika mji wa Othaya, jimbo la Nyeri, Kaskazini mwa mji mkuu wa Kenya, Nairobi.

Marehemu Kibaki alipewa heshima za kijeshi huku akipigiwa mizinga 19, kama njia ya kumuenzi amiri jeshi mkuu wa zamani.

Kabla ya mazishi hayo, ibada ya mwisho iliyohudhuriwa na maelfu ya watu, akiwemo rais wa sasa Uhuru Kenyatta na viongozi wengine wa kisisa, ilifanyika mjini Othaya, ikiongozwa na askofu wa Kanisa Katoliki katika jimbo la Nyeri, Anthony Muheria.

Mwili wa rais huyo wa zamani ulisafirishwa kwa gari kutoka chumba cha kuhifadhi maiti cha Lee mjini Nairobi hadi kwenye uwanja ambako hafla hiyo imefanyika, na Wakenya wengi walionekana wakipiga foleni barabarani wakipungia mkono msafara wake, kama heshima zao za mwisho.

Kibaki ameombolezwa na waliozungumza wakati wa hafla hiyo kama kiongozi aliyebadilisha mkondo wa ustawi wa Kenya, na kuleta matokeo chanya kwa taifa hilo la Afrika Mashariki. Kibaki alifariki akiwa na umri wa miaka 90.

Wachambuzi wanasema Rais Kibaki atakumbukwa Zaidi kwa sera zake zilizoimarisha uchumi na sekta ya elimu nchini Kenya.

Pia atakumbukwa kama rais ambaye utawala wake uligubikwa na tuhuma za ulaji rushwa wa kiwango cha juu, pamoja na kipindi chenye dosari, ya umwagikaji wa damu uliopelekea vifo vya Zaidi ya watu 1,200, na maelfu kufurushwa makwao, kufuatia uchaguzi uliokuwa na utata, wa mwaka wa 2007.

Wakati wa utawala wake, Rwanda na Burundi zilijiunga na jumuiya ya Afrika Mashariki na Sudan Kusini ikapata uhuru wake kutoka kwa Sudan.

"Sudan Kusini iko huru kwa sababu ya Rais Kibaki kwani alijitolea kwa dhati kuhakikisha kwamba tumepata uhuru. Tutamkumbuka daima kwa hilo," alisema Rais Salva Kiir katika hotuba iliyosomwa na mwakilishi wake kwenye hafla iliyofanyika Ijumaa.

Kibaki aliongoza Kenya kati ya mwaka wa 2003 na 2013. Ibada ya kitaifa, ya kumuenzi na kumkumbuka rais huyo wa zamani, ilifanyika jana Ijumaa mjini Nairobi na kuhudhuriwa na viongozi kadhaa, wakiwemo Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, mwenzake wa Syudan Kusini, Salva Kiir, na yule wa Ethiopia, Sahle-Work Zewde.

XS
SM
MD
LG