Rufaa hiyo dhidi ya mkurugenzi huyo iliyofunguliwa katika Mahakama Kuu inahusu kosa la matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali hasara ya Sh.milioni 887.1.
Wakili wa Serikali Leonard Swai alidai kuwa Jamhuri haijaridhika na hukumu hiyo kwamba pamoja na kwamba mikataba inadaiwa kuwa haikufuata sheria lakini mawakili walilipwa fedha ambayo imesababisha hasara chini ya uongozi wa Mhando.
Rufaa hiyo inasubiri kupangiwa jaji na tarehe ya kusikilizwa.
Wiki iliyopita Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam ilimwachia huru aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Mhando, baada ya kukutikana hana hatia.
Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yake juu ya matumizi mabaya ya madaraka na kusababishia serikali hasara.
Katika utetezi wake Mhando alidai kuwa mchakato mzima wa kuingia ubia wa kuhamisha TBC kutoka katika mfumo wa analojia kwenda digitali ulifanywa na bodi ya TBC.
Mahakama hiyo pia imesema kwamba mkataba anaodaiwa kusaini Tido kinyume cha sheria haukidhi vigezo vya kuitwa mikataba.