Magoha amekufa wakati akipatiwa matibabu kwenye hospitali binafsi mjini Nairobi alikokimbizwa baada ya kupata matatizo ya moyo.
Profesa Magoha atakumbukwa kama waziri aliyekuwa na uadilifu mkubwa katika kutekeleza majukumu yake kwenye wizara hiyo. Atakumbukwa pia kwa kuwepo ofisini wakati wa mtaala mpya wa elimu wa CBC na pia alikuwa mstari wa mbele kupanga mikakati ya elimu katika kipindi kigumu cha janga la Covid-19.
Taarifa za kifo chake zimekuja siku chache tu baada ya chuo kikuu cha Maseno kutangaza kwamba angejiunga tena kama profesa wa kufundisha kwenye kitengo cha matibabu.
Kifo chake ni pigo kubwa kwa familia yake kwasababu ndugu yake Profesa Richard Nyabera Magoha alikuwa azikwe Jumamosi wiki hii baada ya kufariki akiwa Marekani Desemba 6, 2022. Mwezi Agosti mwaka uliopita, Magoha alimpoteza ndugu yake mwingine Charles Agunga Magoha aliyefariki akiwa Sweden.