Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 20:20

Jaji Barrett aendelea kuhojiwa na Baraza la Seneti Marekani


Amy Coney Barrett akiwa anahojiwa na Kamati ya Sheria ya Baraza la Seneti (Andrew Caballero-Reynolds/Pool via AP)
Amy Coney Barrett akiwa anahojiwa na Kamati ya Sheria ya Baraza la Seneti (Andrew Caballero-Reynolds/Pool via AP)

Kamati ya Sheria ya Baraza la Seneti Marekani inatarajiwa kumaliza kumhoji Jaji Amy Coney Barrett Alhamisi kabla ya kumidhinisha kuweza kuchukua nafasi katika mahakama kuu iliyoachwa wazi na jaji mashuhuri wa mrengo wa kushoto Ruth Rader Ginsburg aliyefariki mwezi uliopita.

Majaji wa mahakama ya juu hupatiwa nafasi za maisha ambazo zina nguvu kubwa za kisheria na mvutano wa kujaza kiti hicho umekuwa shabaha kubwa katika kampeni kati ya Rais Donald Trump na Mpinzani wake Joe Biden.

Rais Donald Trump (kushoto) na Makamu wa Rais wa zamani Joe Biden
Rais Donald Trump (kushoto) na Makamu wa Rais wa zamani Joe Biden


Wapinzani na waungaji mkono wa Amy Coney Barrett walikuwa wanakutana nje ya jengo la mahakama ya juu hapa Washington mnamo wiki hii nzima.

Jaji huyo mhafidhina anakabiliwa na maswali magumu kutoka kwa Wademocrat, kwa mfano iwapo atajiondoa kwenye kesi ambazo zinaweza kuwa na athari katika matokeo ya uchaguzi wa Novemba.

Barrett Mteule katika mahakama ya juu Marekani anaeleza : "Nitatumia sababu ambazo majaji wengine wanazo mbele yangu kuamua ikiwa mazingira yaliopo yananihitaji kujitoa au la, lakini siwezi kutoa uamuzi wa kisheria hivi sasa juu ya matokeo ya uamuzi ambao nitachukua."

Uteuzi wa majaji wahafidhina ni ahadi muhimu ya kampeni kwa Rais Donald Trump, ambaye mara nyingi huchukulia kwa msimamo wa kiitikadi.

Raid Trump anaeleza : "Kama Joe Biden na Wademokrat watachukuwa madaraka, watajaza mahakama ya juu na watu wenye msimamo mkali wa mrengo wa kushoto ambao watabadilisha kabisa mfumo wa jamii ya Marekani kutoweza kutambulika tena."

Hivi sasa Trump yupo nyuma katika utafiti wa maoni, na mara nyingi anadai njia pekee atakayopoteza dhidi ya mpinzani wake wa chama cha Democratic Joe Biden, ni ikiwa kuna wizi kwenye uchaguzi.

Kukiwepo tayari mashtaka kadhaa yanayohusiana na uchaguzi ambayo yamewasilishwa mahakamani, basi matokeo yanayokaribiana katika majimbo yenye ushindani mkubwa maarufu “Swing State”, yanaweza kumaanisha mazingira kama yale yaliyotokea katika uchaguzi wa mwaka 2000, kati ya George W. Bush na Al Gore, ambapo matokeo yaliamuliwa na kura ya mahakama ya juu Marekani.

Rais wa zamani George W. Bush na Makamu wa Rais wa zamani Albert Arnold Gore
Rais wa zamani George W. Bush na Makamu wa Rais wa zamani Albert Arnold Gore

Kauli za Trump na baadhi ya Warepublikan zinaonyesha kwamba Barrett lazima athibitishwe ili kuhakikisha mahakama inawatolea uamuzi unaowapendelea wao katika kesi za baada ya uchaguzi, hii inaleta sura mbaya alisema mtaalamu wa katiba, Adam White.

White anafafanua : "Kwa kweli wameunda wingu ambalo ninadhani atalazimika kuliondoa wakati wa kazi yake mwenyewe katika mahakama ili kuweka wazi kabisa kwamba akiteuliwa kuchukua nafasi kwenye mahakama, hatokuwa chini ya amri ya Rais Trump au mtu yeyote isipokuwa kufuata sheria peke yake."

Iwapo Barrett atathibitishwa, kutakuwa na majaji sita walioteuliwa na marais wa republican na watatu walioteuliwa na marais wa Democratik.

Kama Biden atashinda, Wademocratik wengine wanamtaka apanuwe nafasi kwenye mahakama hiyo ya juu na kuteuwa majaji zaidi, wakisema kwamba itasaidia kusawazisha msimamo wa kiitikadi katika mahakama. Warepublican wanapinga vikali hilo. Idadi ya majaji haijawekwa kwenye katiba, lakini kumekuwepo na majaji tisa tangu mwaka 1869.

Biden anasema yeye sio shabiki wa kuongeza idadi ya majaji kwenye mahakama, lakini kwa kiasi kikubwa anaepuka suala hilo, akizingatia wasiwasi wa Wademocratik kwamba mahakama inaweza kubatilisha sheria muhimu ya enzi za Obama kuhusiana na huduma nafuu ya afya inayowapatia Wamarekani wengi zaidi fursa ya kupata huduma ya afya.

Rais wa zamani Barack Obama
Rais wa zamani Barack Obama

Biden anaeleza : Jaji Mteule huyu alisema anataka kuondoa sheria ya huduma nafuu ya afya. Rais anataka kuondoa sheria hiyo pia ya huduma nafuu ya afya."

Barrett alisisitiza kwamba ikiwa atathibitishwa hana ajenda yeyote kuhusiana na Obamacare au masuala mengine yanayo sababisha mgawanyiko wa kisiasa, ikiwa ni pamoja na haki za utoaji mimba na ndoa za jinsia moja.

Imetayarishwa na mwandishi wetu Mkamiti Kibayasi, Washington, DC.

XS
SM
MD
LG