Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 10:14

Umoja wa Mataifa yaiomba ICC kuchunguza makosa ya jinai Burundi


Zeid Raad al Hussein
Zeid Raad al Hussein

Baraza la Umoja wa Mataifa la haki za binadamu linaomba mahakama ya makosa ya jinai (ICC ) kuanzisha uchunguzi dhidi ya watuhumiwa wa makosa ya jinai yaliyofanyika nchini Burundi kufuatia mzozo wa kisiasa ulioibuka Aprili 2015.

Watuhimiwa hao wameorodheshwa ndani ya ripoti iliyowekwa hadharani Jumatatu jijini Geneva nchini Uswizi.

Serikali ya Burundi bado haijatoa tamko lolote, lakini tayari tume ya wabunge 12 imekwisha teuliwa kutathmini yaliyomo ndani ya ripoti hiyo.

Mwandishi wa idhaa ya Kiswahili VOA ameripoti kuwa ripoti hiyo iliyowekwahadharani inafuatia mzozo wa kisiasa hapa nchini mara baada ya Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza kutangazwa na chama chake kuwa mgombea urais kwa muhula mwingine.

Watu hao ni baadhi yamaafisa serikalini, pamoja pia na wajumbe wa tawi la vijana wafuasi wa chama tawala maarufu kama Imbonerakure.

Watalaam waliofanya utafiti juu maovu na ukiukwaji wa haki za binadamu yaliofanyika nchini Burundi tangu mwaka 2015 wamemkabidhi majina hayo Kamishna Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu, Zeid Raad al Hussein.

Ripoti hiyo inasema kuwa visa vya utekaji nyara, mauaji, ubakaji, na kuwafunga watu kwa misingi ya kisiasa vilifanywa na watu hao hapa Burundi tangu April 2015. Hata hivyo watalamu wa Umoja wa Mataifa waliofanya utafiti huo wanahakikisha kuwa na wapinzani wa serikali walifanya makosa yanayodhalilisha watu lakini kwamba walikosa ushahidi wa kutoka katika utafiti wao.

Watalaam watatu walioendesha utafiti huo katika ripoti hiyo wanaomba serikali kufuta waranti za kimataifa zilizotolewa kwa wanasiasa wa uponzani na watetezi wa haki za binadamu waliotoroka nchi.Wanaomba pia serikali irejeshe uhusiano wake na ofisi na kamishna mkuu wa haki za binadamu uliyositishwa kuanzia septemba mwaka jana, wanaozuiliwa kwa misingi ya kisiasa waachiliwe huru.

Wakati Burundi inakaribia kuvunja uhusiano wake na mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai ICC baadaye mwezi ujao, watalamu hao wanaomba Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuiomba mahakama hiyo ifanye uchunguzi wa makosa ya jinai yaliyofanyika hapa nchini.

Ripoti hii inatarajiwa pia kuonyeshwa katika kikao cha wajumbe wa baraza la Umoja wa Mataifa la haki za binadamu ambao watakuwa mjini Geneva katika kikao chao cha 36 kuanzia tarehe 11 hadi 29 mwezi huu.

Haya yanajiri huku upande wa serikali Ijumaa iliyopita, bunge la taifa liliwateuwa wajumbe 12 wa tume ambayo ilipewa jukumu la kutathimini yaliyomo ndani ya ripoti hiyo.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Haidallah Hakizimana, Burundi

XS
SM
MD
LG