Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 12:29

Idara ya Usalama ya Russia zafunga uchunguzi dhidi ya Wagner


Yevgeny Prigozhin
Yevgeny Prigozhin

Idara ya Usalama ya Serikali Kuu ya Russia imetangaza Jumanne inafunga uchunguzi kuhusu uasi wa kutumia silaha uliofanywa na Yevgeny Prigozhin na wapiganaji wa kikundi chake cha mamluki cha Wagner.

Katika taarifa iliyochapishwa na mashirika mbalimbali ya habari nchini Russia, FSB ilisema wale waliohusika “walisitisha harakati zilizokuwa zimeelekezwa kutekeleza uhalifu huo.”

Kutowafungulia mashtaka wapiganaji hao ilikuwa ni sehemu ya makubaliano yaliyofikiwa Jumamosi jioni ambayo yalipelekea kusitishwa kwa uasi huo.

Kikundi cha mamluki wa Wagner wakiondoka kutoka katika kambi ya jeshi ya wilaya ya kusini waliokuwa wanaishikilia kwa muda Juni 24, 2023.
Kikundi cha mamluki wa Wagner wakiondoka kutoka katika kambi ya jeshi ya wilaya ya kusini waliokuwa wanaishikilia kwa muda Juni 24, 2023.

Wizara ya Ulinzi ya Russia pia ilisema Jumanne kuwa kikundi cha Wagner kilikuwa kinajitayarisha kukabidhi vifaa muhimu vya kijeshi kwa jeshi la Russia.

Mpaka leo Jumanne haiko wazi mahali aliko Prigozhin.

Tovuti zinazofuatilia safari za ndege zilionyesha ndege inayohusishwa na Prigozhin ilitua Belarus Jumanne.

Kiongozi wa Wagner alisema atakwenda Belarus ikiwa ni sehemu ya makubaliano yaliyofikiwa na kiongozi wa Belarus Alexander Lukashenko kumaliza uasi huo.

Hotuba ya Putin

Katika hotuba yake kwa taifa la Russia, Rais wa Russia Vladimir Putin Jumatatu aliwakaripia walioandaa uasi uliofanywa na wapiganaji wa Wagner, akiwaita “wasaliti.”

Kiongozi huyo wa Russia alisema waandaaji hao waliwaambia uongo watu wao na “kuwasukuma katika kifo, chini ya mashambulizi, kujipiga risasi wenyewe, “kuwabadilishia mwelekeo wapiganaji wa Wagner’ wakikiri kosa la kuuvamia mji wa kusini wa Rostov, ambo waliukamata kwa muda wakiwa wanaelekea Moscow,

Rais wa Russia Vladimir Putin
Rais wa Russia Vladimir Putin

Putin aliwakaribisha wapiganaji wa Wagner na makamanda wao, ambao aliwaita mashujaa akiwataka wajiunge na jeshi la Russia kwa kusaini makubaliano na Wizara ya Ulinzi ya Russia au na idara nyingine za usalama.

Pia aliwaambia wanahiari iwapo wanataka kwenda kujiunga na familia zao na marafiki au kwenda kuishi Belarus iwapo watachagua hilo.

Kiongozi huyo wa Russia hakumtaja kabisa Prigozhin. Lakini alisema waandaaji wa uasi huo waliisaliti nchi yao, watu wao na kuwapotosha wale waliotumbukia katika uhalifu huo.

Baadhi ya taarifa katika habari hii zinatokana na mashirika ya habari ya AP, AFP na Reuters.

Forum

XS
SM
MD
LG