Rais wa Marekani Barack Obama amesema nchi yake ilijiunga katika kampeni za kijeshi za mataifa ya magharibi dhidi ya kiongozi wa Libya Moammar Gadhafi, kuzuia mauaji na kumaliza utawala unaokandamiza watu wa Libya.
Katika hotuba yake kwa taifa iliyotangazwa kwenye televisheni, amesema kuwa kampeni hizo zilizohalalishwa na Umoja wa Mataifa zimezuia mauaji ya raia kutoka kwa kiongozi huyo wa Libya.
Rais amesema kuwa Bw. Gadhafi amepoteza imani kwa watu wake na haki ya kuongoza, na kuongeza kuwa “hakuna shaka kuwa Libya, na dunia kwa ujumla, itakuwa salama zaidi “ ikiwa Bw. Gadhafi hatokuwa madarakani.
Lakini akasema kuwa kupanua harakati za kijeshi na kujumuisha mabadiliko ya utawala nchini Libya litakuwa ni kosa.
Bw. Obama pia alizungumzia umuhimu wa kumzuia Bw. Gadhafi kuwaadhibu wale wanaompinga, jambo ambalo linaweza kusababisha kile ambacho kingeonekana kama mgogoro wa kibinadamu.
Akizungumza na sauti ya Amerika, mara baada ya hotuba hiyo, Prof. Ladi Madosh Makene wa Chuo kikuu cha Clark mjini Boston alisema rais Obama ametetea vyema maamuzi ya utawala wake na kujaribu kutuliza wakosoaji wake juu ya hatua aliyochukua ya kijeshi dhidi ya Moammar Ghadafi.