Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 08:05

Hatua ya Ruto kutangaza nafasi za makamishna wa IEBC yaibua utata


Mgombea urais wa Kenya Raila Odinga akipokelewa na IEBC
Mgombea urais wa Kenya Raila Odinga akipokelewa na IEBC

Rais wa Kenya William Ruto ametangaza wazi nafasi sita katika Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC, wakati bado jopo la watu tisa alilounda kuwachunguza makamishna wanne wa tume hiyo waliopinga ushindi wake katika uchaguzi wa urais wa Agosti 9, linaendelea na uchunguzi.

Kupitia chapisho kwenye Gazeti rasmi la serikali Jumanne, Ruto ametangaza nafasi ya mwenyekiti wa tume hiyo ya uchaguzi na makamishna watano kuwa wazi, kupisha rasmi mchakato wa kuajiriwa kwa makamishna wapya wa tume hiyo.

“HIVYO SASA, kwa kutumia mamlaka niliyopewa na kifungu cha 7A (2) cha Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, 2011 kama inavyosomwa na Ibara ya 1 (1) ya Sheria hiyo, mimi, William Samoei Ruto, Rais wa Jamhuri ya Kenya na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, natangaza wazi nafasi katika nafasi za Mwenyekiti na makamishna watano wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka,” sehemu ya chapisho hilo inasoma.

Mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati tayari ameondoka afisini baada ya kustaafu pamoja na makamishna wengine wawili—Boya Molu na Prof Abdi Guliye—baada ya kuhudumu kwa miaka sita.

Watatu hao walistaafu mnano Januari 17, 2023 wakati tume hiyo ilikuwa haina kamishana yeyote anayehudumu kufuatia kufurushwa kwa makamishna wengine wanne waliopinga kutangazwa kwa William Ruto kuwa mshindi wa kura ya Urais ya Agosti 9, mwaka uliopita.

Rais Ruto alitangazwa kuwa mshindi wa kura ya urais kwa kujizolea 50.49% ya kura zote za urais dhidi ya mpinzani wake wa karibu aliyeungwa mkono na rais mstaafu Uhuru Kenyatta, ambaye ni Bw Odinga aliyejizolea asilimia 48.5%. Hata hivyo, Odinga alielekea mahakamani kupinga uhalali wa matokeo ya kura hiyo ya urais, lakini majaji saba wa mahakama ya juu nchini Kenya, kwa kauli moja walitupilia mbali pingamizi hilo, kwa kauli kuwa uchaguzi huo uliafiki viwango vya kisheria kwa mujibu wa Kifungu cha 138 (3) (c) na 138 (10) cha katiba ya Kenya na kwamba Ruto, alitangazwa inavyostahili kwa kupata kura asilimia 50%+1 ya kura zote zilizopigwa.

Hata hivyo, Odinga ametangaza kuwa hamtambui Ruto kuwa rais na kumtaka aondoke ofisini kwa “kutochaguliwa kwa njia halali”

Nafasi nyingine zilizotangazwa wazi ni za makamu mwenyekiti wa tume hiyo Juliana Cherera, makamishna Justus Nyang’aya na Francis Wanderi wote walijiuzulu hata kabla ya jopo hilo kutayarisha utaratibu wa awali wa vikao vyake.

Jopo hilo la wanachama tisa lililoundwa na rais Ruto na kuongozwa na jaji wa mahakama ya rufaa Aggrey Muchelule, lilianza vikao vyake wiki chache baada ya bunge la Kenya kuidhinisha ripoti ya mapendekezo ya Kamati ya Bunge ya Sheria , iliyosikiliza maombi manne ya kutaka kubanduliwa kwao kwa madai ya kuonesha utovu wa nidhamu, utepetevu kazini, ukosefu wa uadilifu katika afisi ya umma na kujihusisha na mkakati unaomithilishwa na mapinduzi ya Katiba ya Kenya na kuvunja imani ya raia wa Kenya, wapiga kura walipopinga ushindi wa rais William Ruto katika uchaguzi wa Agosti 9.

Kando na kumchunguza Kamishna Irene Masit, ambaye amekataa kujizulu wadhifa huo, jopo hilo limeeleza kuwa litawachunguza makamishna wote wanne kwa madai ya kuonesha utovu wa nidhamu, utepetevu kazini, ukosefu wa uadilifu katika afisi ya umma na kujihusisha na mkakati unaomithilishwa na mapinduzi ya Katiba ya Kenya na kuvunja imani ya raia wa Kenya, wapiga.

Bunge la Kenya tayari limepitisha Mswada wa marekebisho wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) nambari 49 ya 2022 bila marekebisho yoyote kufanyika, na kuweka mwanga wa muundo wa jopo la uteuzi ili kuwaajiri makamishna wapya wa tume hiyo ya uchaguzi.

Mswada huo ambao umesainiwa kuwa sheria unapendekeza jopo la uteuzi wa makamishna wapya wa IEBC kuwa na watu saba, wawakilishi wawili wa tume ya huduma kwa bunge, tume ya utumishi wa umma kuwa na mwakilishi mmoja, chama cha mawakili nchini Kenya kutoa mwakilishi mmoja, baraza la kidini kutoa wakilishi wawili na mwakilishi mmoja aliyependekezwa na Kamati ya Uhusiano ya Vyama vya Siasa nchini Kenya.

Kwa mujibu wa Kifungu cha 7A (2) cha Sheria ya IEBC, Rais anastahili kutangaza nafasi katika tume hiyo ndani ya kipindi cha siku saba baada ya kutokea kwa nafasi katika afisi ya mwenyekiti au makamishna wa tume.

Na vile vile, Rais, angalau miezi sita kabla ya kumalizika kwa muhula wa mwenyekiti au kamishana wa tume au ndani ya siku 14 baada ya kutangazwa kwa nafasi katika ofisi ya mwenyekiti au kamishna wa tume, anastahili, kupitia gazeti rasmi la serikali kutangaza uteuzi wa jopo litakalotwikwa jukumu la kuwaajiri makamishana wapya wa tume hiyo baada ya mchakato wa mahojiano ya umma.

Kutokana na hatua ya rais ya Jumanne ya kutangaza wazi nafasi hizo, wakati wowote anatarajiwa kutangaza uteuzi wa jopo la uteuzi la watu saba kuelekeza mchakato wa kuwateua makamishna wapya wa tume ya uchaguzi.

IMETAYARISHWA NA KENNEDY WANDERA, SAUTI YA AMERIKA, NAIROBI.

XS
SM
MD
LG