Kidero ambaye ni mojawapo wa viongozi maarufu ambao wamefikishwa mahakamani, ameshtakiwa kwa kutumia madaraka yake vibaya na vile vile kula njama na maafisa wengine waliokuwa wakisimamia jimbo hilo.
Kwa mujibu wa uchunguzi amesababisha kupotea kwa takriban shilingi milioni laki mbili. Na japo amekanusha mashtaka hayo, mawakili wake wameieleza mahakama kuwa mashtaka yanayomkabili Kidero ni ya kisiasa.
Wakati huo huo, siku sijazo maafisa zaidi, wakiwemo magavana wanatarajiwa kufikishwa kizimbani kujibu mashtaka ya ubadhirifu wa fedha za umma.
Matumizi mabaya ya madaraka
Mwandishi wa idhaa ya Kiswahili VOA anaripoti kuwa Kidero aliyekamatwa Jumatano jioni baada ya kujisalimisha mbele ya tume ya kupambana na ufisadi amesomewa mashtaka ya matumizi mabaya ya madaraka, kushirikiana na watu wengine kutekeleza ufisadi, kulipa makampuni mamilioni ya fedha kwa huduma zisizokuwepo.
Kati ya Januari 16, 2014 na Januari 25, 2016, Kidero na maafisa wengine nane wa jimbo la jiji la Nairobi wanatuhumiwa kuipora serikali ya jimbo hilo kiwango cha fedha cha shilingi milioni laki mbili na kumi na tatu.
Pia anatuhumiwa kuwa Kidero alipokea shilingi milioni ishirini na nne kutoka kwa kampuni iitwayo Lodwar Wholesalers Ltd kama rushwa.
Tume ya kupambana na rushwa
Tume ya kupambana na ufisadi (EACC) ilieleza awali kuwa imekuwa ikifanya uchunguzi kubaini madai kuwa gavana huyu amehusika katika ubadhirifu wa fedha za umma.
Na baada ya kuikabidhi idara ya kuendesha mashtaka ya umma stakabadhi zilizo na mapendekezo, Mkurugenzi wa idara hiyo Noordin Haji alithibitisha Jumatano kuwa upo ushahidi wa kutosha kumshtaki gavana huyu na maafisa wengine waliohudumu katika serikali ya jimbo la Nairobi.
Wakili adai ni Tuhuma za kisiasa
Hata hivyo, Tom Ojienda, wakili wa Kidero ameieleza mahakama inayosikiliza kesi za ufisadi chini ya hakimu Douglas Ogoti kuwa mashtaka aliyosomewa Kidero ni ya kisiasa.
Ojienda amesema: "Haya si mashtaka yenye msingi wowote. Ni mashtaka tu ya kawaida. Haya yanayofungamana na siasa. Mahakama hii ni sharti iingilie kati wakati yapo mashtaka ya kisiasa kwenye mkondo huu wa kisheria. Pale ambapo pana siasa, mahakama iingilie kati."
Na kwa madai ya mawakili wa watuhumiwa kuwa upande wa mashtaka ulichukua muda mwingi kabla ya kuwafikisha watuhumiwa mahakamani, mawakili wa serikali wajitetea kuwa walichukua muda unaostahili.
Mwanasiasa huyo ambaye ameachiliwa kwa dhamana taslimu ya shilingi milioni mbili, Machi mwaka huu alitajwa na ripoti ya kampuni ya KPMG iliyofanya ukaguzi wa utawala wake na kueleza kuwa takriban shilingi bilioni ishirini na moja hazihesabiwi kwenye akaunti za jimbo.
Imetayarishwa na Mwandishi wetu Kennedy Wandera, Kenya