Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Novemba 05, 2024 Local time: 06:26

EU yashutumiwa vikali kwa kuiondolea Burundi vikwazo


Ramani ya Burundi.
Ramani ya Burundi.

Mashirika mbalimbali ya kiraia nchini Burundi yameisuta jumuiya ya Umoja wa Ulaya kufuatia uamuzi wake wa kurejesha msaada wa kifedha kwa nchi hiyo, yakisema serikali bado inaminya haki za binadamu.

Hatua ya Jumanne ya Umoja wa Ulaya ilifuatia uamuzi sawa na huo wa Marekani mwaka jana, huku Brussels ikisema kuna " matumaini" kufuatia uchaguzi wa mwaka 2020, ambao ulimweka madarakani Rais Evariste Ndayishimiye.

Lakini tamko lililotiwa saini na zaidi ya mashirika 15 ya kutetea haki za Burundi walio uhamishoni na makundi mengine ya kutetea haki yalisema "yanachukizwa" na kuondolewa kwa vikwazo hivyo.

Mnamo mwaka wa 2016, Umoja wa Ulaya, wakati huo mfadhili mkuu wa misaada wa Burundi, ulikuwa umesitisha ufadhili wote wa moja kwa moja kwa serikali kutokana na rekodi yake ya haki na kwa kushindwa kuzuia wimbi kubwa la vurugu.

Burundi ilikumbwa na msukosuko wakati rais wa wakati huo Pierre Nkurunziza aliposhinda muhula wa tatu ambao upinzani ulidai kuwa ni kinyume cha sheria.

Machafuko hayo yalisababisha vifo vya Warundi 1,200 na kupelekea 400,000 kukimbia, huku kukiwa na taarifa za kukamatwa kiholela, mauaji na kupotea kwa watu.

"Hali tuliyoikimbia bado ni ile ile leo," alilalamika Dieudonne Bashirashize kutoka shirika la CAVIB, mmoja wa waliotia saini taarifa hiyo.

"Kuondolewa kwa vikwazo kuna hatari ya kuwa na matokeo mabaya sana," aliongeza, akielezea hofu kwamba serikali itaiona hatua hiyo ya Umoja wa Ulaya kama kuunga mkono sera zake za ukandamizaji.

Taarifa hiyo iliitaka EU kwendelea na vikwazo kwa watu binafsi wanaokiuka haki na kushinikiza mamlaka ya Burundi kufanya uchunguzi huru haraka kuhusu ukiukaji ulioripotiwa.

Pia ilitoa wito kwa mashirika ya kiraia ya kimataifa na ya ndani na waandishi wa habari waweze "kufanya kazi kwa uhuru nchini Burundi, bila kuhofia usalama wao".

EU ilisema Jumanne uamuzi wake wa kuondoa vikwazo hivyo ulitokana na "mchakato wa amani wa kisiasa ulioanza na uchaguzi mkuu wa Mei 2020 na ambao umefungua dirisha jipya la matumaini kwa wakazi wa Burundi".

Hata hivyo ilikiri kwamba "changamoto zimesalia katika nyanja za haki za binadamu, utawala bora, maridhiano na utawala wa sheria".

Tume ya Uchunguzi ya Umoja wa Mataifa ilisema mwezi Septemba kwamba hali ya haki imezorota tangu Ndayishimiye achukue mamlaka mnamo Juni 2020.

"Wanachama wa vyama vya upinzani... bado wanalengwa mara kwa mara na vitendo vya dhuluma na wanakabiliwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu kama vile kupotea, kukamatwa kiholela na kuwekwa kizuizini na kuteswa," ilisema ripoti hiyo.

Wakati huo huo, Jumuiya ya Afrika Mashariki imefurahishwa na hatua ya Umoja wa Ulaya kuiondolea Burundi vikwazo hivyo vya kiuchumi.

Katibu mkuu wa jumuiya hiyo, Peter Mathuki, amesema kwamba hatua hiyo ya umoja wa ulaya inatarajiwa kufufua ukuaji wa uchumi nchini Burundi na kuchochea ushirikiano wa maendeleo katika jumuiya ya Afrika mashariki.

Umoja wa ulaya unafadhili miradi ya biashara, utawala, amani, usalama, kuhifadhi mazingira na mabadiliko ya hali ya hewa, katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika mashariki.

Mathuki amesema kwamba miradi hiyo itaimarika zaidi kufuatia hatua hiyo.

XS
SM
MD
LG