Ndege ya shirika la ndege la Ethiopia ilituma picha kwa njia ya Tweet ikionyesha ndege Boeing 787 Dreamliner ikiruka katika safari yake fupi kutoka Addis Ababa kwenda Asmara ikiwa na maelezo “Ndege ya amani imeruka kuelekea #Asmara! #Familyreunion#Ethiopia #Eritrea"
Abiria waliokuwa katika ndege hiyo ni pamoja na waziri mkuu wa Ethiopia Haliemariam Desalegn, ambaye alikuwa akiongeza kundi hilo la wasafiri. Waliwekewa zulia jekundu wakati walipowasili uwanja wa ndege wa asmara, kwa mujibu wa maelezo ya mwandishi wa VOA.
Kuanzishwa kwa safari ya ndege ni ukurasa mpya na zama za kurudisha uhusiano kwa haraka ambao ulianzishwa na waziri mkuu anayependa mageuzi, Abiy Ahmed, aliyetangaza mwezi Juni kuwa Addis Ababa hatimaye itaheshimu makubaliano yaliyosainiwa mwaka 2000 kumaliza vita vya miaka miwili vya mpakana vilivyouwa takriban watu 70,000.
Mapema mwezi huu, Ahmed na Rais wa Eritrea Isaias Afwerki walisaini makubaliano ya amani ya kihistoria ambayo yalimaliza moja ya migogoro sugu ya muda mrefu.
Mataifa hayo mawili tangia kufikia makubaliano yamerejesha huduma za simu, na Eritrea imefungua ubalozi wake Addis Ababa Jumatatu.
Eritrea ilikuwa ni jimbo la zamani la Ethiopia mpaka lilipojitenga na kutangaza uhuru wake mwaka 1993.