Mkutano huo wa pamoja uliofanyika jijini Dar es Salaam, Tanzania,uliohudhuriwa na wakuu wa nchi na serikali kutoka mataifa wanachama wa EACna SADC, uliongozwa na Mwenyekiti wa EAC, Rais wa Kenya Dkt. William Ruto, na Mwenyekiti wa SADC, Rais wa Zimbabwe Dkt. Emmerson Mnangagwa.
Baada ya majadiliano ya kina, viongozi wa EAC na SADC wamekubaliana kuwa mgogoro wa mashariki mwa DRC unaweza kutatuliwa kwa njia ya kisiasa,kidiplomasia, na hatua za kiusalama.
Akisoma maazimio ya Mkutano huo Katibu Mkuu wa EAC, Veronica Nduva alisema mkutano umeamua kuwa pande zote zinazozozana katika mgogoro huo zisitishe mapigano mara moja na kuweka silaha chini bila masharti yoyote.
Viongozi wamesisitiza kuwa njia za misaada ya kibinadamu lazima zifunguliwe haraka ili kuruhusu upatikanaji wa chakula, dawa, na huduma nyingine muhimu kwa wananchi walioathiriwa na mapigano.
Ili kuhakikisha hali ya usalama inarejea, wakuu wa majeshi wa EAC na SADC wamepewa siku tano kuandaa mpango wa ulinzi wa Goma na maeneo yanayozunguka jiji hilo. Hatua hii inalenga kuzuia mashambulizi zaidi na kuwalinda wananchi walio katika hatari ya kushambuliwa na waasi.
Katibu Mkuu huyo alisema kwa upande wa mazungumzo ya amani, viongozi wa EAC na SADC wameamua kuwa serikali ya DRC irejee kwenye meza ya mazungumzo na makundi yote, yakiwemo ya kijeshi na yasiyo ya kijeshi, chini ya mwavuli wa mchakato wa Nairobi na Luanda.
Wamekubaliana pia kuwa juhudi zote za amani zinazofanyika ziunganishwe kuwa mpango mmoja ili kuharakisha upatikanaji wa suluhu yakudumu.
Viongozi wa mkutano huo wameagiza kuondolewa kwa vikosi vyote vya kigeni visivyoalikwa kutoka ardhi ya DRC. Ili kuhakikisha utekelezaji wa hatua hiyo, wameagiza kufanyika kwa kikao cha pamoja cha Mawaziri wa Ulinzi wa EAC na SADC ndani ya siku 30 zijazo ili kuweka mkakati madhubuti wa utekelezaji.
Pamoja na hayo, viongozi hao wamesisitiza kuwa suluhisho la kudumu kwamgogoro wa DRC lazima lijikite katika ushirikiano wa kisiasa na kidiplomasia.Wamesisitiza kuwa jumuiya ya kimataifa pia inapaswa kuunga mkono juhudi zakuleta amani, hasa kwa kusaidia juhudi za kidiplomasia na kuzuia uungwaji mkonowa makundi ya waasi.
Mkutano huo pia umeazimia kuwa vikao vya aina hiyo viwe vinafanyika angalau mara moja kwa mwaka ili kujadili maendeleo ya utekelezaji wa maazimio yaliyowekwa na kuhakikisha kuwa mchakato wa kurejesha amani DRC unaendelea kwa kasi inayotakiwa.
Ripoti ya Amri Ramadhani, Sauti ya Amerika, Dar es Salaam.
Forum