Akifungua jopo la ushirikiano kati ya China na Afrika mjini Bejing, Jumatatu, Rais Xi aliwambia viongozi wa Afrika kwamba uwekezaji wa China haufunganishwi na masharti ya kisiasa na wala nchi yake haina nia ya kuingilia kati masuala ya ndani ya Afrika.
Rais Xi aliahidi kutoa dola bilioni 60 kusaidia misaada ya maendeleo kwa miaka mitatu ijayo. Dola bilioni 15, kati ya hizo ni msaada wa bure bila ya riba kwa lengo la kupunguza wasiwasi kwamba msaada wa China unazitumbukiza nchi za Afrika katika madeni zaidi.
Viongozi na wakuu wa serikali za nchi za Afrika wanaohudhuria mkutano huo unaofanyika kila mwaka wanasifu jukumu muhimu la China katika maendeleo ya nchi zao na kueleza kwamba Bejing inashirikiana na nchi zote za Afrika kwa usawa na heshima.
Rais wa Africa Kusini Cyril Ramaphosa aliyekuwa mwenyekiti wa jopo lililopita, amesema kwamba China ni mshirika mkuu wa nchi za Afrika na inachukua jukumu muhimu kuzisaidia nchi hizo kuimarisha maendeleo na uchumi wao kama mshirika wa sawa.
Kabla ya ufunguzi wa mkutano wa kilele Jumatatu, Marais Xi na Ramaphosa waliongoza mkutano wa viongozi juu ya namna ya kuimarisha uchumi na ushirikiano wa kibiashara kati ya pande hizo mbili.
Imetayarishwa na Mwandishi wetu Abdushakur Aboud, Washington, DC.