Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 04:45

Bobi Wine: Mimi siyo pekee niliyeteswa na kikosi cha Museveni


Kikosi cha usalama kikiwazuia waandamanaji Uganda, Agosti 31, 2018
Kikosi cha usalama kikiwazuia waandamanaji Uganda, Agosti 31, 2018

Mbunge wa Uganda Bobi Wine, amesisitiza kwamba bado anahisi maumivu makali baada ya kupigwa vibaya na wanajeshi wanaomlinda Rais Yoweri Museveni.

Bobi Wine, ameeleza masikitiko yake dhidi ya serikali ya Uganda, Alhamisi, mjini Washington, DC, Marekani, akieleza wanafanya ujanja kukwepa madai ya kumtesa, bila kuzingatia kwamba siyo pekee aliyepigwa na kuumizwa na maafisa wa jeshi.

Bobi Wine amesisitiza kwamba atarudi nyumbani baada ya matibabu na hataogopa kuendelea na harakati za kupigania haki na demokrasia nchini mwake.

Mwandishi wa idhaa ya Kiswahili VOA anaripoti kuwa alionekana mnyonge akitembea polepole sana na kutumia mkongojo maalum, huku akisaidiwa na mawakili wake.

Kwa mara ya kwanza, tangu alipo kamatwa na kufunguliwa mashtaka ya kupanga njama za kuipindua serikali ya Rais Yoweri Museveni, BobI Wine ameelezea yaliyo mkuta mikononi mwa maafisa wa jeshi wanaotoa ulinzi kwa Rais.

Bila kutaka kueleza mengi, uso wake ukionekana kuwa na alama za kupigwa na mikono iliyochubuka ngozi, Bobi Wine amesema alipigwa vibaya na maafisa hao.

Bobi Wine, hata hivyo amesisitiza kwamba kupigwa kwake na kufunguliwa mashtaka ya uhaini, hakutamzuia kuendelea kupigania haki za raia wa Uganda, demokraisa na mfumo wa utawala unaoheshimu haki za kibinadamu, akisisitiza kwamba atarejea nyumbani kwa kufuata ushauri wa daktari mara tu atakapo maliza matibabu.

Amesisitiza kwamba sababu yake kubwa ya kusafiri kuja Marekani kwa matibabu zaidi ni kutokana na kukosa imani na aina ya dawa iliyo tumika kumtibu wakati alikuwa anazuiliwa na maafisa wa jeshi.

Mawakili wake nao wanasema kwamba wanakusanya taarifa zote za dhuluma dhidi ya raia wa Uganda zinazodaiwa kutekelezwa na utawala wa rais Museveni, na kuziasilisha kwa wafadhili wa Uganda, kwa lengo la kutaka ufadhili huo kusimamishwa hadi hali utawala utakapoheshimu haki za kibinadamu.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Kennes Bwire, Washington, DC.

XS
SM
MD
LG