Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 16:07

Bobi Wine amdadisi Balozi kwa nini Uganda 'inawatesa' wananchi wake


Mbunge wa Uganda Bobi Wine
Mbunge wa Uganda Bobi Wine

Mvutano baina ya Balozi wa Uganda nchini Marekani, Mull Sebujja Katende, na Mbunge Robert Kyagulanyi ulijitokeza Jumatano, wakati wa mahojiano kwenye kipindi cha VOA - Straight Talk Africa, mjini Washington, Marekani ambapo mbunge amemdadisi balozi ni kwa nini serikali ya Uganda 'inawatesa' wananchi wake.

Wakati wa mahojiano hayo Kyagulani maarufu kama Bobi Wine katika madai yake ameishutumu serikali ya Uganda kwa kuwatesa wananchi akionyesha yeye jinsi alivyoteswa baada ya kukamatwa na kikosi maalum cha kumlinda Rais Museveni, huku kwa upande wake Balozi Katende akisisitiza kuwa Uganda ni nchi inayo heshimu mfumo wa demokrasia, sheria na haki za kibinadamu.

Katika mahojiano hayo Balozi Katende, na Mbunge Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine, walitofautiana kuhusu hali ya siasa, haki na sheria nchini Uganda, mbele ya mwendeshaji wa kipindi hicho shaka Ssali.

Bobi Wine ambaye yupo nchini Marekani kwa matibabu baada ya kupata majeraha akiwa mikononi mwa kikosi maalum cha jeshi kufuatia kukamatwa kwake huko Arua mwezi Agosti, 2018 na kuteswa.

Kwa upande wake Balozi amekanusha kuwa Uganda haiungi mkono mateso.

Amesema kuwa chochote kilichomtokea wakati alipokamatwa, vyombo vya usalama, nchini Uganda, vinafanya uchunguzi juu ya madai ya Bob Wine juu ya mateso aliyo yapata na hivyo akitaka wasubiri matokeo ya uchunguzi huo mpaka yatakapo fikishwa mahakamani.

Balozi Katende, amesema kinacho endelea Uganda wale wapinzani ambao wana maoni tofauti, ambao wameshindwa kuwashawishi wananchi kuwapa kura kuingia katika bunge, wanaishia kufikiria kuwa njia mbadala iliyo bora ni kusababisha fujo na wapate ushindi kupitia machafuko ya kisiasa.

Ameongeza kuwa Bobi Wine hana haki ya kuzungumza kwa niaba ya raia wa Uganda kwa sababu anawakilisha jimbo moja tu, na kwamba aliye na haki ya kuzungumza kwa niaba ya taifa hilo ni Rais Yoweri Museveni.

Lakini Bobi Wine, alimkabili balozi Katende akidai kuwa Uganda inaongozwa kwa utawala wa kiimla, usiomruhusu mtu yeyote kumkosoa Rais Museveni.

Bobi Wine alitaka kujua kutoka kwa balozi ni kwa nini yeye akiwa mwananchi wa Uganda abambikiziwe kesi ya kumiliki bunduki mbili na risasi kadhaa, na baadaye mashtaka yafutwe katika mazingira tatanishi bila kueleza nani mmiliki wa bunduki hizo, na bunduki zenyewe kutoweka.

Bobi Wine pia alikanusha madai ya serikali ya Uganda kwamba yeye na wenzake wanatumiwa na nchi za nje.

“Siko hapa kwa ajili ya kuwakilisha upinzani, lakini ni kwa ajili ya wananchi wa Uganda. Kwa taarifa yako sikiwakilishi chama chochote cha siasa hapa bali nina wakilisha wananchi wa Uganda na hasa watu wa kizazi changu,” amesisitiza.

“Nafanya kazi yangu kwa ajili ya nchi yangu Uganda. Nimezaliwa na kukuzwa katika mitaa duni nikiishi katika mabanda na Mungu amenisaidia kufika hapa nilipo kwenye studio za VOA kupitia msaada wa wananchi wenzangu,” Bobi Wine amesisitiza.

Mwanasiasa huyo ameongeza : “Nguvu hiyo ndio inayonifanya nizungumze kwa niaba ya raia wa Uganda bila uoga wala upendeleo bila ya kujali anayeumizwa na ukweli wangu.”

"Malengo yetu ni makubwa kuliko Muhozi, mtoto wa Museveni, hao wachache waliobahatika kuzaliwa katika maisha bora. Lengo letu ni kuwanufaisha walio wengi ambao wanaishi maisha ya shida.

Wasichana niliozaliwa wakati moja nao wanakufa wakizaa, vijana waliozaliwa katika zama zangu wanateseka gerezani bila kufikishwa mahakamani,” alisema Bobi Wine.

Muda mfupi baada ya kipindi cha Straight Talk Africa kuanza kupeperushwa, umeme ulizimika sehemu kubwa nchini Uganda na raia kubaki gizani hivyo kushindwa kufuatilia kipindi hicho.

Shirika la umeme la Uganda lilitoa tangazo kuwaarifu wateja wake kuwa umeme umekatika nchi nzima na shirika hilo linafanya juhudi za kuurejesha. Vyombo vya habari nchini Uganda viliripoti baadaye kuwa huduma za umeme zilirejea muda mfupi baada ya baada ya kipindi cha Straight Talk kumalizika.

Rais wa Uganda Yoweri Museeveni, anatarajiwa kuhutubia taifa jumamosi, hii ikiwa mara ya pili katika kipindi cha wiki moja, na mara ya nane, tangu mbunge Bobi Wine alipokamatwa na kufunguliwa mashtaka ya uhaini nchini humo.

XS
SM
MD
LG