Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Desemba 25, 2024 Local time: 07:38

Benki Kuu ya Nigeria yafichua sakata ya udanganyifu ya dola bilioni 2.4


Rais wa Nigeria Bola Tinubu (Katikati)
Rais wa Nigeria Bola Tinubu (Katikati)

Benki kuu ya Nigeria wiki hii imesema kwamba imegundua fedha za kigeni zenye thamani ya dola bilioni 2.4 ambazo zinaitishwa kwa njia ya udanganyifu, kufuatia uchunguzi wa dola bilioni 7 zilizokuwa zikisubiri kukabidhiwa wenyewe.

Benki hiyo imesema kwamba ufichuzi huo utapunguza changamoto zilizosababishwa na uhaba wa fedha za kigeni nchini, ikidai kuwa madai kwa njia ya udanganyifu huenda yakaathiri uchumi wa Nigeria.

Ungunduzi huo ni kufuatia uchunguzi wa kina uliofanywa na kampuni ya kimataifa ya kifedha ya Deloitte kwa niaba ya Benki Kuu ya Nigeria.

Benki hiyo imesema kwamba ufichuzi huo ni wa kutisha, wakati kukiwa na stakabadhi bandia, watu wasiokuwepo na wanaodai fedha za kigeni, na wakati mwingine watu ambao wamepokea fedha za kigeni bila kutoa maombi rasmi.

Ripoti zimeongeza kuwa baadhi ya watu pia walipokea zaidi ya fedha za kigeni walizoitisha kutoka benki hiyo. Gavana wa benki hiyo Olayemi Cardoso amesema kwamba hawatatoa fedha kwa maombi yasio halali, wakati mchambuzi wa masuala ya kiuchumi Ogho Okiti akisema kwamba hiyo ni hatua kuelekea njia inayofaa.

"Tunapiga hatua zifaazo, ikizingatiwa kuwa sasa tayari tumeshugulikia takraban asilimia 50 ya maombi, ikibaki asilimia sawa na hiyo. Hilo litakapokamilika, tutaweza kuimarisha viwango vya fedha zetu. Nafikiri ni vyema kuwajibisha kila atayepatikana akiwa na nia ya kuibia Benki kuu," Okiti alisema.

Hii ni mara ya kwanza ndani ya miaka 7 kwa hesabu za benki kuu kutolewa kwa umma. Nigeria imekuwa ikikabiliwa na uhaba mkubwa wa fedha za kigeni, suala ambalo limedumaza ukuaji wa kiuchumi, kushuka kwa dhamani ya naira, pamoja na mfumuko wa bei za bidhaa.

Kufikia sasa benki kuu ya Nigeria imelipa takriban dola bilioni 2.3 zinazoitishwa, zikiwemo zile zinazoitishwa na mashirika ya ndege pamoja na sekta za viwanda na nishati.

Mwanauchumi na mratibu wa Kituo cha Haki za Kijamii Justice Eze Onyekprere anasema kwamba ufichuzi uliofanywa hautasaidia kufufua uchumi wa Nigeria.

"Kuna madeni mengine yaliopo, Hilo halitatatua lolote. Kiwango cha sarafu kwa upande wa thamani kimezidi sera za fedha za benki kuu. Inahusiana zaidi na suala la uongozi, kwenye makadirio, viwanda, elimu na sera za afya. Ulisikia gavana wa benki kuu akieleza bunge kwamba utalii wa afya pamoja na ulipaji wake wa ada ulitumia takriban dola bilioni 40 ndani ya kipindi cha miaka 10. Hiyo ni sawa na takriban dola bilioni 4 kila mwaka," alisema.

Hata hivyo Onyekpere anasema kwamba ufichuzi huo inaashiria matatizo zaidi kwenye mfumo wa fedha za kigeni wa Nigeria, ambayo yanahitaji kushugulikiwa.

Baada ya kuchukua usukani mwaka jana, rais Bola Tinubu aliapa kuangamiza ufisadi wakati pia akifanya marekebisho ili kuinua uchumi. Kufikia sasa hakuna lililofanyika, wakati wa Nigeria wakiendelea kusubiri.

Forum

XS
SM
MD
LG