Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Januari 28, 2025 Local time: 05:13

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa laomba M23 kusitisha mashambulizi mashariki mwa DRC


Balozi wa Marekani na naibu mwakilishi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Dorothy Camille Shea akizungumza kwenye mkutano wa Baraza la Usalama mjini New York, Januari 26, 2025. Picha ya AP
Balozi wa Marekani na naibu mwakilishi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Dorothy Camille Shea akizungumza kwenye mkutano wa Baraza la Usalama mjini New York, Januari 26, 2025. Picha ya AP

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Jumapili limewataka waasi wa M23 kusitisha mashambulizi yao na kuacha kusonga mbele kuelekea mji wa Goma, mji mkubwa wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na kuomba majeshi ya kigeni kuondoka mara moja.

Ombi hilo la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linajiri saa chache baada ya waasi wa M23 kudai kwamba wamechukua udhibiti wa Goma kufuatia kusonga mbele kwao, hali ambayo ilisababisha maelfu ya watu kukimbia na kuzua wasiwasi wa kutokea vita vya kikanda.

Baraza hilo lenye wanachama 15 lilikutana mapema Jumapili kujadili mzozo huo na kisha kukubaliana kwa kauli moja.

Baraza hilo limezitaka Rwanda na DRC kurudi kwenye meza ya mazungumzo ili kufikia amani na kushughulikia masuala yanayohusu kuwepo kwa jeshi la Rwanda katika eneo la mashariki mwa Congo na uungaji mkono wa Congo kwa waasi wa Rwanda wa FDLR.

M23 inaapa kulinda maslahi ya Watutsi, hasa dhidi ya wanamgambo wa Kihutu kama vile FDLR, ambayo ilianzishwa na Wahutu waliotoroka Rwanda baada ya kushiriki katika mauaji ya kimbari ya zaidi ya Watutsi 800,000 na Wahutu wenye msimamo wa wastani mwaka 1994.

Katika mkutano wa Baraza hilo Jumapili, Marekani, Ufaransa na Uingereza zimelaani kile walichosema ni uungaji mkono wa Rwanda kwa waasi wa M23. Kigali ilikanusha kwa muda mrefu kuunga mkono M23.

Forum

XS
SM
MD
LG